Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imewasimamisha watoa huduma wawili wa vifaa vya kufuatilia mwenendo wa mabasi ambao vifaa vyao vimebainika kuchezewa. Watoa huduma hao ni Utrack Africa Ltd na Easy Track Solution JV RJ Motchand Ltd.
Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 11, 2023 katika ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu LATRA CPA Habibu Suluo amesema kampuni hizo zilifanyiwa tathmini kwa mujibu wa Mkataba ambapo Mamlaka ilibaini mapungufu yasiyovumilika.
“Kampuni hizi mbili ndizo zilizofunga kifaa cha kufuatilia mwenendo wa magari (VTD) kwenye mabasi 27 ambayo yamefungiwa kwa mwezi Machi, 2023. Kwa sasa zinatakiwa kurekebisha kasoro zilizobainika kwenye mabasi yaliyofungiwa na wakikamilisha watarudishwa kuendelea na utoaji wa huduma ya kufunga vifaa vipya,”ameeleza CPA Suluo.
LATRA iliingia Mkataba na Watoa Huduma watano (5) ambazo ni kampuni zilizochaguliwa kwa mchakato wa zabuni wa kufunga vifaa vya kufuatilia mwenendo wa magari (VTDs) ambao ni Fleet Truck, Tera Technologies, Easy Truck, Utruck na ICTPack.