Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA YAWATAKA WADAU KUTEKELEZA KANUNI ZA MFUMO WA VTS
Imewekwa: 27 Jul, 2024
LATRA YAWATAKA WADAU KUTEKELEZA KANUNI ZA MFUMO WA VTS

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imewataka watoa huduma wa vifaa vya kufuatilia mwenendo wa vyombo vya usafiri (VTD) kutekeleza Kanuni za Mfumo wa Ufuatiliaji Mwenendo wa Vyombo vya Usafiri (VTS) za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini za Mwaka 2024 ili kuboresha huduma za usafirishaji pamoja na kusambaza vifaa vya VTD vyenye ubora na tija katika sekta ya usafirishaji.

Hayo yamebainishwa na Bi. Halima Lutavi, Meneja Ufuatiliaji Usafiri wa Barabara LATRA alipotoa elimu ya Kanuni za VTS kwa watoa huduma wa VTD katika kikao cha pamoja kati ya LATRA na watoa huduma hao kilichofanyika katika ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam Julai 26, 2024.

Aidha, Bi. Halima amesema watoa huduma hao wa VTD wamepitishwa kwenye maeneo yote ya Kanuni hizo za VTS kwa lengo la kuwaongezea uelewa ili watekeleze majukumu yao kwa uweledi na ufanisi kama inavyoelekezwa kwenye Kanuni hizo.

Vilevile Bi. Lutavi amewaasa watoa huduma hao kuendelea kuzisoma na kuzielewa vizuri Kanuni hizo na amesisistiza kuwa, endapo Mamlaka itabaini kuwa Kanuni hizo hazifuatwi, itachukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kumsimamishia mtoa huduma.

“Hakikisheni mnakuwa na mafundi wenye uweledi na uzoefu ili waweze kuhudumia kifaa kwa ufanisi wa hali ya juu na pia muhakikishe mafundi wenu wana sare na kitambulisho ili waweze kutambulika pale wanapotakiwa kutoa huduma”, ameeleza Bi. Halima.

Aidha, ameongeza kuwa, “Mamlaka inawakaribisha watoa huduma kutoka kampuni mbalimbali ambazo zina uwezo wa kutoa huduma hiyo kwa ufanisi na wanaweza wakafanya maombi ya cheti cha idhini kutoka LATRA kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa na baada ya Mamlaka kujiridhisha kuwa mtoa huduma anaweza kufanya kazi kwa weledi basi ataidhinishwa na kupatiwa cheti cha idhini ya kutoa huduma hiyo.”

Naye. Bw. Geofrey Silanda, Meneja Uratibu Usalama na Mazingira LATRA amesema kuwa, Mamlaka imejipanga kuwasimamia na kufanya ufuatiliaji wa karibu kwa watoa huduma wa vifaa vya VTD, “Sisi kama Mamlaka tutahakikisha tunakagua vifaa hivi vizuri na tukigundua kuwa vifaa havifanyi kazi baada ya kuvifanyia majaribio Mamlaka itampatia mtoa huduma huyo siku 14 kubadilisha kifaa na kukifanyia marekebisho na akishindwa kufanya hivyo tutampa siku 30 na akishindwa kutekeleza basi Mamlaka haitompatia kibali cha kufunga kifaa hicho.”

Kwa upande wake, Wakili Abasi Msuya kutoka TERA Tecknologies ameishukuru Mamlaka kwa ushirikiano mzuri uliopo na kwa kupatiwa elimu ya Kanuni hizo ambazo zitakuwa ni nyenzo nzuri wanapotekeleza majukumu yao, na amewasihi watoa huduma za VTD kuzingatia Kanuni zilizowekwa.

Naye Bw. Christopher Mbagwa, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Dar es Salaam (VETA) amesema kuwa, kupitia Kanuni hizi itasaidia kutatua changamoto zinazojitokeza barabarani kwani itasaidia pia uwepo wa mafundi wenye uweledi.

“Nimepokea elimu hii kwa mtazamo chanya ukizingatia usafiri ni jambo muhimu kwa kila Mtanzania na zipo changamoto nyingi zinajitokeza barabarani hivyo kupitia Kanuni hizi changamoto zitatatuliwa na sisi VETA tutawawezesha mafundi kuwa na ujuzi mzuri wa kutengeneza vifaa hivi, vilevile ninawaasa wasambazaji wa vifaa hivi kutumia vifaa vyenye ubora,” amesema Bw. Mbagwa.

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo