Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA: ZINGATIENI SHERIA ZA USALAMA BARABARANI
Imewekwa: 22 Jun, 2023
LATRA: ZINGATIENI SHERIA ZA USALAMA BARABARANI

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imewasihi watumiaji wa huduma za usafiri ardhini kufuata Sheria, kanuni na Taratibu za Usalama Barabarani ili kuepuka ajali na madhila mengine yanayoweza kutokea.

Hayo yamesemwa na Bw. Salum Pazzy, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kutoka LATRA  wakati wafanyakazi wa LATRA walipotembelea Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI) na kushiriki zoezi la Uchangiaji Damu ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Juni 21, 2023.

Akizungumza baada ya kuchangia damu Bw. Pazzy amesema baadhi ya watumiaji wa huduma za usafiri ardhini wamekuwa na tabia ya kupuuzia Sheria za Usalama Barabarani na wengine kushabikia uvunjifu wa Sheria hizo, hali inayowaweka katika hatari ya kupata ajali na madhila mengine barabarani.

“Ningependa kuwasihi wasafirishaji na watumiaji wengine wa huduma za usafiri ardhini kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za Usalama Barabarani, kwani kwa kufanya hivyo wanaweza kujiepusha na changamoto mbalimbali wawapo safarini kama ambavyo tumeshuhudia wenzetu ambao wapo hapa hospitali kwa sababu ya ajali,  hivyo ni vyema kujiepusha na tabia hatarishi pamoja na kushabikia tabia hizo,” amesema Bw. Pazzy.

Akizungumzia sababu za LATRA kwenda katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI) Bw. Jonathan Kitururu, Mratibu wa Pikipiki za magurudumu mawili na matatu kutoka LATRA amesema wahanga wengi wa ajali za barabarani wanatibiwa MOI hivyo imekuwa rahisi kuwafikia na kuwapa faraja.

“Asilimia kubwa ya waathirika wa ajali za barabarani ni bodaboda na bajaji, hivyo watu hawa ni wahitaji haswa wa damu na wanatuhusu moja kwa moja, hivyo tukaona ni vyema kuja hapa (MOI) na kushiriki zoezi la kuchangia damu,” amesema BW. Kitururu.

Naye Bw. Patrick Mvungi, Meneja Uhusiano kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) amewashukuru wafanyakazi wa LATRA kwa kufika na kushiriki zoezi la kuchangia damu huku akiwaasa wananchi wengine kujitokeza na kuchangia damu kwani kwa kufanya hivyo wanasaidia kuokoa maisha.

“Tnawashukuru sana ndugu zetu wa LATRA waliotenga muda wao kufika hapa (MOI) na kushiriki zoezi la kuchangia damu kwaajili ya kusaidia wagonjwa wetu. Hapa MOI mahitaji ya damu ni makubwa sana wastani wa chupa 15 hadi 30 kwa siku, ukizingatia kwamba tunapokea idadi kubwa ya majeruhi wanaohitaji kufanyiwa upasuaji na kuongezewa damu, hivyo nitoe wito kwa Taasisi nyingine na Watanzania kwa jumla kujitokeza na kuchangia damu kwani kwa kufanya hivyo tunaokoa maisha ya watu wengi,” amesema Bw. Mvungi.

Akizungumza baada ya kuchangia damu Bi. Lilian Temu, Afisa Huduma kwa Wateja LATRA ameelezea hali aliyoipitia wakati akichangia damu, “Nimefurahi sana kuchangia damu naamini itaokoa maisha ya mtu, hii ni mara yangu ya kwanza kuchangia damu, mwanzoni nilikuwa na hofu sana, niliwaza labda nitapata kizunguzungu au nitadondoka au hata kuugua, lakini baada ya kuchangia damu hofu yote imeondoka na ninajiona ni mzima kabisa, hivyo watu waache uoga na wajitokeze wachangie damuz,” amesema Bi. Lilian.

Asilimia kubwa ya ajali za barabarani zinasababishwa na makosa ya kibinadamu kama vile mwendokasi uliopitiliza na kupuuzia alama za barabarani, madhara ya ajali hizo husababisha kupoteza maisha au kupoteza viungo vya mwili na hivyo kupoteza nguvu kazi ya Taifa. Hivyo ni vyema kwa watumiaji wa huduma za usafiri ardhini kufuata Sheria za Usalama Barabarani na kuacha kushabikia uvunjaji wa Sheria hizo ili kufanya Usafiri Ardhini kuwa salama.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo