Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imefungia leseni za usafirishaji abiria kwa mabasi 22 kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Februari, 2023 kutokana na kosa la madereva wa mabasi hayo kuchezea na kuharibu Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS).
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara kutoka LATRA Bw. Johansen Kahatano, kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Februari 21,2023 katika ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam.
Bw. Kahatano amesema Mamlaka imechukua hatua ya kufungia leseni za usafirishaji kwa mabasi hayo ndani ya mwezi mmoja kama adhabu kutokana na makosa mbalimbali yaliyofanywa na madereva wa mabasi hayo ili madereva waweze kujirekebisha.
“Tumebaini mabasi yapatayo 22 yameharibiwa mfumo wa kufuatilia mwenendo wa mabasi barabarani (VTS) iwe ni wamiliki wenyewe au madereva, njia ambayo wanaitumia ni kuua betri ili kuwawezesha kuwasha na kuzima vifaa hivyo kwa muda wanaotaka wao, hali inayosababisha mfumo kutotuma taarifa au kutuma taarifa isiyokamilika, hivyo tumechukua hatua ya kuyafungia kwa muda wa mwezi mmoja ili wajirekebishe," amesema Bw. Kahatano.
Aidha, Bw. Kahatano ameongezea kuwa LATRA imekubaliana na Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua za Kisheria wamiliki wa mabasi kwa kufungia leseni lakini pia madereva wa basi husika nao wachukuliwe hatua za Kisheria kwa uvunjifu wa Sheria za Usalama Barabarani.
“Mamlaka kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi tunadhibiti kila upande ili kuhakikisha kwamba madereva wana sehemu yao ya kuwajibika lakini pia wamiliki wa magari wana sehemu yao ya kuwajibika," ameongeza Bw. Kahatano
Bw. Kahatano amewakumbusha wasafirishaji wenye nia njema na mfumo wa VTS kuwa, wanaweza kufuatilia mabasi yao kupitia simu zao za mkononi ili waweze kuangalia mwenendo mzima wa mabasi yao na kuona taarifa zote wakati mabasi yakiwa safarini kwani wamepatiwa akaunti zao ambazo zimeunganishwa na mfumo wa VTS moja kwa moja.
Ikumbukwe kuwa uharibifu wa mfumo wa VTS ni ukiukwaji wa kanuni ya 51 ya Kanuni za Leseni za Usafirishaji za mwaka 2020, hivyo ni wito kwa wamiliki wa mabasi na madereva kuzingatia Sheria na Kanuni zilizowekwa ili kuhakikisha usalama barabarani, kwa wasafirishaji na abiria kwa jumla.