Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MABASI 27 YAFUNGIWA
Imewekwa: 11 Apr, 2023
MABASI 27 YAFUNGIWA

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imesitisha leseni za usafirishaji abiria kwa mabasi 27 kwa kipindi cha mwezi Machi, 2023.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu LATRA CPA Habibu Suluo alipozungumza na waandishi wa habari Aprili 11, 2023 katika ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam.

CPA Suluo amesema uamuzi huo umefanyika kwa mujibu wa Kifungu cha 5(1)(b) ya Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura ya 413 na Kanuni ya 27(1)(c) na (d) ya Kanuni za Leseni za Usafirishaji (Magari ya Abiria) za Mwaka 2020.

“Hatua hii ni kutokana na vitendo vya kuingilia Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) na kusababisha mfumo kutotuma taarifa kabisa ama kutuma taarifa kwa kurukaruka (skipping). Hapa kuna baadhi ya mabasi ambayo baada ya wataalamu wa Mamlaka kufanya uchunguzi, waligundua betri za vifaa vya kufuatilia mwenendo wa mabasi (VTDs) zimeharibiwa na mifumo yake ya umeme kubadilishwa,” amefafanua CPA Suluo.

Vilevile amesema kuwa, kuna mabasi ambayo yamekutwa yakiwa na mfumo wenye swichi inayotumiwa na dereva kuzima na kuwasha kifaa hicho (VTD) na hatari zaidi ni kwamba yapo mabasi ambayo yamebadilishwa mfumo (software) na kutuma taarifa za uongo kwenye kituo cha ufuatiliaji wa mwenendo wa magari.

“Ninawasihi madereva na wasafirishaji wote kuacha tabia hii mara moja na wafahamu kuwa mfumo wa VTS una uwezo wa kutoa taarifa kwa Mamlaka iwapo utaingiliwa au kuharibiwa, tutaendelea kutoa adhabu kwa wale wote wanaofanya vitendo hivi ambavyo havikubaliki na vinahatarisha maisha ya watanzania wanasafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine,” amesisitiza CPA Suluo.

Aidha, CPA Suluo ameeleza kuwa, kitendo cha kuingilia Mfumo wa VTS ni ukiukwaji wa Kanuni ya 51(a) na (b) ya Kanuni za Leseni za Usafirishaji (Magari ya Abiria) za Mwaka 2020 ambapo Kanuni ya 51(a) inamtaka mmiliki (mwenye leseni) ahakikishe basi lake limefungwa kifaa cha kufuatili gari (installed with VTD), kiwe kinafanyakazi vyema (working properly), kinafanyiwa marekebisho (maintained), kinakingwa na mazingira hatarishi (protected against hazardous conditions) na hakichezewi (tempering).

Pia, Kanuni ya 51(b) inaelekeza “kifaa chochote cha ufuatiliaji wa magari (VTD) kitakapokuwa hakifanyi kazi ipasavyo (any malfunctions of VTD) kitolewe taarifa kwa Mamlaka ndani ya saa 12 (reported to the Authority within twelve hours).

“Katika barua zetu za kusitisha leseni hizi, tuliwaelekeza wamiliki wa mabasi husika, kabla hatujaondoa sitisho letu, wafanye marekebisho ya mfumo na kujiridhisha unafanya kazi vyema kisha wawasilishe uthibitisho wa marekebisho hayo. Pia tumewaelekeza kuwafikisha madereva husika Jeshi la Polisi kwa hatua zingine chini ya Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168,” amesisitiza CPA Suluo.

Wakati huohuo CPA Suluo amewasihi na kuwakumbusha wamiliki au watoa huduma ambao wamesitishiwa leseni za magari yao kuzingatia Sheria na Kanuni katika utoaji wa huduma kwa umma na amewasihi kuajiri watu wenye weledi na mahiri watakaoweza kuwasaidia kusimamia huduma ya usafirishaji na kuwashauri ipasavyo ili kuboresha huduma kwa wateja, kukuza mitaji na biashara zao.

Vilevile amesema, “Mtakapoona maamuzi yetu kama Mdhibiti sio sahihi, Sheria inataka mje kwetu kupinga maamuzi hayo kwa hoja na kuna Jopo la Mapitio (Review Panel) ya Bodi itafanya kazi yake na kutoa maamuzi, Na endapo hujaridhika na maamuzi ya Jopo, basi hatua inayofuata ni kwenda kwenye Baraza la Ushindani (Fair Competition Tribunal).”

Pakua orodha ya mabasi yaliyofungiwa

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo