Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MABASI YA NEW FORCE KUANZA SAFARI SAA 9 USIKU NA 11 ALFAJIRI
Imewekwa: 08 Sep, 2023
MABASI YA NEW FORCE KUANZA SAFARI SAA 9 USIKU NA 11 ALFAJIRI

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imerudisha ratiba na leseni za mabasi 38 ya kampuni ya New Force kuanzia tarehe 11 Septemba, 2023. Mabasi hayo yataanza safari zake muda wa 9.00 usiku na saa 11.00 alfajiri.

Hayo yamebainishwa na Bw. Johansen Kahatano, Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara kutoka LATRA kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Septemba 8, 2023 katika ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam.

Bw. Jahatano amesema kuwa LATRA imefikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha kuwa kampuni hiyo imetekeleza maelekezo iliyowapatia hapo awali ikiwemo kuhakikisha wanazingatia muda wa kuanza safari, kutafuta mshauri mwelekezi kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa uongozi wa kampuni na madereva kuhusu Sheria za Usalama Barabarani na Udereva wa Kujihami and udhibiti wa uchovu pamoja na kuhakikisha kuwa madereva wote wanasajiliwa kwenye mfumo wa ufuatiliaji mwenendo wa magari (VTS), kuwa na i-button na kusajiliwa kwenye mfumo wa uthibitisho wa madereva.

“Tumepokea taarifa ya mafunzo yaliyotolewa kwa madera 50 wa kampuni hiyo kwa kuona vyeti vya kuhitimu mafunzo, tumepokea orodha ya wadhamini wa madereva hao kuwa wamesoma wameelewa na watazingatia Sheria zote za Usalama Barabarani katika kutoa huduma za usafirishaji abiria na tumefuatilia kwenye mfumo wa VTS mabasi yote ya kampuni hiyo kwa kipindi chote cha adhabu na kujiridhisha kuwa uvunjifu wa ratiba kwa kutoka kabla ya muda na mwendo kasi umedhibitiwa. Hii ni dalili njema kwa uongozi na madera wa kampuni hii kutii Sheria,” ameeleza Kahatano.

Vilevile ameeleza kuwa, kutolewa kwa ruhusa hiyo iwe ni fundisho kwa kampuni ya New Force na wasafirishaji wote wanaokiuka Sheria, Kanuni na Taratibu za Usalama Barabarani na Mamlaka haitasita kuchukua hatua stahiki kwa yeyote atakayevunja Sheria na Taratibu zilizowekwa.

Naye Bw. Masumbuko Masuke, Meneja wa Kampuni ya New Force amesema, "Tunaishukuru LATRA na Jeshi la Polisi kwa kutupatia elimu ya Usalama Barabarani na tunaahidikutekeleza Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo. Tunawaomba radhi abiria wetu kwa yote yaliyotokea na niwahakikishie kuwa kwa sasa tumebadilika, tutazingatia yote tuliyoelekezwa."

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo