
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imewahimiza madereva wa vyombo vya moto kibiashara kujisajili na kuthibitishwa na LATRA kama illivyoainishwa kwenye Kanuni ya (4)(1) ya Uthibitishaji wa Madereva na Usajili wa Wahudumu ya mwaka 2020.
Bw. Omary Saleh, Afisa Mfawidhi LATRA Mkoa wa Arusha amesema hayo hivi karibuni alipotoa elimu ya usajili na uthibitishaji wa madereva wa vyombo vya moto kibiashara jijini Arusha.
“Taratibu za kusajiliwa ni rahisi sana kama unasimu janja unaweza kuingia katika Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Barabara na Reli (RRIMS) na utaingiza taarifa zako za NIDA kisha utaambatisha cheti cha udereva na leseni ya udereva. Lengo ni kupata taarifa za kumbukumbu za madereva waliosajiliwa na kuthibitishwa na LATRA na Mamlaka itaweza kutambua makosa ya dereva husika anayeendesha chombo kwa wakati huo,” ameeleza Bw. Saleh.
Vilevile Bw. Saleh ameeleza kuwa Mamlaka imeweka mazingira rafiki yanayomuwezesha dereva kufanya mtihani wa uthibitishaji, “Utaratibu uliowekwa kulingana na mazingira Serikali imezingatia ambapo mtihani huo hufanywa kwa lugha mama ya kiswahili ili madereva wapate kuelewa na maswali yanayoulizwa ni ya kupima uelewa wa dereva na mfumo ni rahisi unaomuwezesha dereva kujibu maswali bila kupata changamoto yoyote.”
Pia, Bw. Saleh alitoa elimu ya matumizi sahihi ya Kitufe cha Utambuzi wa Dereva i- Button) kwa madereva wa magari maalum ya kukodi (Special Hire) wanachopatiwa baada ya kuthibitishwa na Mamlaka ambapo amewaeleza madereva hao kuwa i-Button ni mali ya dereva na sio mmiliki na wanapaswa kukitumia wakati wote wa safari ili kupata taarifa za dereva husika pamoja na kutambua mwenendo wake akiwa safarini.
Naye Bw. Ernest Mmasi, dereva wa mabasi ya mjini (daladala) kituo cha daladala Kilombero Jijini Arusha ameishukuru Mamlaka kwa jitihada za kuwapatia elimu ya usajili na uthibitishaji na wameona ni jambo lenye tija na litawaongezea heshima na kutanua wigo wa ajira ya fani hiyo.
“Jambo hili lilikuwa linanitatiza kwa kuwa hatukuwa na uelewa wa kwanini tunalazimika kufanya mtihani wa LATRA hali ya kuwa madereva wameshafanya mtihani wa VETA na kupatiwa leseni halali, baada ya kupata elimu hii kwa sasa nimeelewa na nitakuwa balozi mzuri kwa wenzangu kwa kuwahamasisha kwenda ofisi za LATRA na kufanya mtihani wa uelewa na hatimaye na sisi tuthibitishwe na kutambulika na Serikali,” amesema Bw. Mmasi.
Bw. Salum Kondo, dereva wa lori Jijini Arusha amewaasa madereva wenzake kwenda kusoma elimu ya udereva kwenye vyuo vinavyotambulika na Serikali ili wapate vyeti vya taaluma hiyo na hatimaye waende LATRA kwa ajili ya kuthibitishwa.
Kwa upande wake, Bw. Humphrey Pallanjo, dereva wa magari maalum ya kukodi jijini Arusha ambaye amesajiliwa na kuthibitishwa na LATRA amesema mtihani wa LATRA sio mgumu jambo la muhimu ni kufanya maandalizi ya kutosha kwa kujisomea na kujikumbusha yale uliyoyasoma chuoni.
Naye Bw. Salum Kivuyo dereva wa magari maalum ya kukodi Arusha amewasihi madereva wa magari maalumu ya kukodi kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Usafiri Ardhini ikiwemo kutumia kwa usahihi kitufe cha utambuzi wa dereva (i-Button) kwa kuwa manufaa yake ni makubwa hasa kwa upande wa usalama wa safari.
Mamlaka inaendelea kuwahimiza madereva wa vyombo vya moto kibiashara kusajiliwa ili kuthibitishwa kwa kuwa jambo hilo ni la kisheria lakini pia linaongeza thamani ya fani yao ya udereva. Baada ya kuthibitishwa, dereva atapatiwa cheti kinachotambulika kitaifa na kimataifa hasa kwa nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), hivyo ni manufaa makubwa kwa kuwa wanaenda kutanua wigo wa ajira ndani na nje ya nchi hatimaye watajiinua kiuchumi na kijamii.