Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MADEREVA DODOMA WAASWA KUSAJILIWA NA KUTHIBITISHWA NA LATRA
Imewekwa: 10 Feb, 2025
MADEREVA DODOMA WAASWA KUSAJILIWA NA KUTHIBITISHWA NA LATRA

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imewaasa madereva wa vyombo vya moto kibiashara kujisajili na kuthibitishwa na LATRA kama illivyoainishwa kwenye Kanuni ya (4)(1) ya Uthibitishaji wa Madereva na Usajili wa Wahudumu ya mwaka 2020.

Hayo yamebainishwa na Bw. Ezekiel Emmanuely, Afisa Mfawidhi LATRA Mkoa wa Dodoma alipotoa elimu ya uthibitishaji wa madereva na usajili wa wahudumu kwa madereva wa magari maalum ya kukodi (Special hire) jijini Dodoma Februari 07, 2025.

“Ni kosa la kisheria kuendesha basi bila kuthibitishwa na Mamlaka, hivyo nitoe wito kwa madereva na wahudumu wa mabasi Tanzania kutii Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa na Serikali ikiwa ni pamoja na kufika ofisi za LATRA zilizo karibu yao kwa ajili ya kuthibitishwa na kusajiliwa”, amesema Bw. Ezekiel.

Naye Bw. Humphrey Ngweta, kiongozi wa Ulinzi na Usalama wa magari maalum ya kukodi jijini Dodoma amesema, “Naishukuru LATRA kwa kutufuata eneo letu la kazi na  kutupatia elimu hii na hivyo niwaombe madereva wenzangu kujitokeza kwa wingi ofisi za LATRA ili tufanye kazi zetu kwa misingi ya Sheria zilizowekwa  kuepuka kuchukuliwa hatua,” ameeleza Bw. Hamphrey

Kwa upande wake Bw.Yusuph Lukungu, dereva wa magari maalum ya kukodi anaeleza tija ya elimu aliyoipata na kumpelekea kuhamasika kusajiliwa na LATRA katika kituo chake cha kazi jijini Dodoma.

 “Kujisajili sio suala gumu kama nilivyokuwa nafikiria cha msingi uwe na cheti chako cha chuo ulichosomea, kitambulisho chako cha NIDA pamoja na leseni yako, jambo hili nimelikamilisha leo, na ninaishukuru sana Serikali kupitia LATRA kwa jitihada ya kuhimiza madereva kujitokeza kwa wingi kusajiliwa ili kuheshimisha kada udereva hapa nchini,” amesisitiza Bw. Lukungu.

Serikali imeweka nia thabiti ya kuitambua kazi nzuri inayotekelezwa na madereva wa vyombo vinayodhibitiwa na LATRA, hivyo suala la uthibitishaji wa madereva na usajili wa wahudumu linaenda kuipa thamani tasnia ya udereva pamoja na kuwaongezea wigo wa ajira kwa kuwa cheti cha uthibitishaji cha LATRA kinatoa fursa kwa madereva kupata ajira ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo