Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

LATRA Logo

MADEREVA MBEYA NA RUKWA WAPEWA ELIMU YA UTHIBITISHAJI WA MADEREVA
Imewekwa: 22 Nov, 2022
MADEREVA MBEYA NA RUKWA WAPEWA ELIMU YA UTHIBITISHAJI WA MADEREVA

Na Mambwana Jumbe

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kupitia Afisa Mfawidhi Mkoa wa Rukwa Bw. Athumani Nyiga pamoja na Afisa Mfawidhi Mkoa wa Mbeya Bw. Omary Saleh imetoa elimu ya Uthibitishaji wa Madereva kwa madereva wa vyombo vya usafiri kibiashara katika mikoa hiyo kwa lengo la kuwafahamisha umuhimu wa kuthibitishwa na LATRA kama ilivyoainishwa kwenye Sheria ya LATRA Sura ya 413.

Akizungumza na madereva kuhusu umuhimu wa kuthibitishwa na LATRA, Bw. Saleh amewaambia kuwa uthibitishaji unayofanywa na Mamlaka itaifanya tasnia ya udereva hapa nchini kuheshimika na kutambulika kama zilivyo kazi nyingine na hivyo kuongeza thamani ya dereva mmoja mmoja hapa nchini, vilevile dereva huyo anaposajiliwa na kuthibitishwa atakuwa na wigo mpana wa kufanya kazi kwenye nchi za Afrika kwa kuwa atatambulika kwenye nchi wanachama za EAC, COMESA na SADC.

"Nadhani wote tunajua mtu ukisimama na kusema mimi ni dereva picha zinazojengeka vichwani mwa watu, ni tofauti na mtu akisimama na kusema mimi ni rubani au hata mimi ni nahodha wa meli. Sasa tutakapokuthibitisha wewe kama dereva unaenda kuheshimika katika kazi yako,"alisema Bw. Saleh.

Naye Afisa Mfawidhi Mkoa wa Rukwa Bw. Athumani Nyiga aliwaambia madereva haokuwa suala laUthibitishaji ni la Kisheria na hivyo amewasihi madereva hao kujisajili kwa kutumia namba yake ya NIDA kwenye mfumo mama wa RRIMS kupitia anuani ya https://rrims.latra.go.tz/ login na kuweka nafasi ya kufanya mtihani (booking) na kisha kuchagua tarehe na muda atakaopenda kufanya mtihani.

Naye Bw. Pascal Mwantosya, mara baada ya kupatiwa elimu hiyo alisema,"Elimu mliyotupatia leo ni muhimu sana na sisi madereva tukithibitishwa hakika sekta yetu ya udereva itakuwa katika hali nzuri na ya heshima. Pia kupitia kuthibitishwa naona madereva tutakuwa makini tunapokuwa kwenye majukumu yetu na hii itasaidia kupunguza ajali kwa kiasi kikubwa. Mimi nipo tayari kuthibitishwa."

Kwa upande wake Bw. David Ndunguru dereva wa magari makubwa ya mizigo amewahimiza madereva wengine kujitokeza kwa lengo la kusajiliwa na kuthibitishwa na LATRA kwa kuwa ni jambo lenye manufaa zaidi kwao.

"Kutokana na elimu tuliyopewa nimegundua kuwa dereva akishathibitishwa anakuwa ametambulika rasmi na anaweza kufanya kazi popote ndani na nje ya nchi. Hivyo ninawashauri madereva wengine tuungane kwa pamoja ili tudhibitishwe" aliongeza Bw. Ndunguru.

Suala la uthibitishaji wa madereva lipo kisheria ambapo kwa mujibu wa Sheria ya LATRA Sura ya 413(5e), LATRA imepewa jukumu la kuwasajili na kuwathibitisha Madereva na Wahudumu wa Vyombo vya Usafiri Kibiashara. Hadi kufikia Novemba 2022, zaidi ya madereva 700 wameshafanya mtihani kwa lengo la kuthibitishwa.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo