Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MADEREVA NA WAMILIKI WAHAMASISHWA KUJIUNGA NA VYAMA VYA USHIRIKA
Imewekwa: 03 Apr, 2025
MADEREVA NA WAMILIKI WAHAMASISHWA KUJIUNGA NA VYAMA VYA USHIRIKA

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imewahamasisha wamiliki na madereva wa pikipiki za magurumu mawili (Bodadoda), pikipiki za magurudumu matatu (Bajaji) pamoja na magari ya mijini (Daladala) kuanzisha vyama vya ushirika kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.

Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Bw. Omary Saleh, Afisa Mfawidhi LATRA Mkoa wa Arusha alipowatembelea wadau hao na kuwapatia elimu ya taratibu na umuhimu wa kujiunga na vyama vya ushirika.

Bw. Saleh amewaeleza wadau hao kwamba, kwenye huduma ya usafirishaji Serikali imewaletea ushirikishaji wa pamoja ambao utawasaidia kufanya mambo makubwa kwa pamoja ikiwemo kuboresha sekta ya usafirishaji na kukuza uchumi wa mmoja mmoja.

“Niwasihi tuungane na tushirikiane kufanikisha jambo hili lenye manufaa makubwa kwa kila mmoja wetu ukizingatia kuwa suala hili la ushirika limeletwa na viongozi wetu na kuwafikia ninyi kwa kuwashirikisha ili mkiona linafaa lifanyiwe kazi kwa kuweka utaratibu mzuri kwa Mamlaka na kwenu wadau kwa kufuata vigezo kama vile kuzingatia huduma inayotolewa kwa pamoja,” amesema Bw. Saleh.

Naye Bw. Pascal John, Afisa Usajili wa ushirika kutoka jiji la Arusha amebainisha taratibu za kufuata kujisajili kwenye umoja wa vyama vya ushirika, “Jambo la ushirika linataratibu zake na sisi tumekamilisha taratibu hizi ikiwemo kuwa na wazo la ushirika na kuwapatia elimu ya ushirika vilevile kuna vigezo vya kuzingatia ili kujiunga kwenye ushirika ikiwemo chama kuwa na washirika wasiopungua idadi ya watu 20 na wawe katika eneo husika kwa pamoja”.

Kwa upande wake Bw. Okelo Constantine, Mwenyekiti Umoja wa Bodaboda Mkoa wa Arusha (UBOMA) amesema kuwa, suala la ushirika kwa Mkoa wa Arusha wamelipokea vizuri na wanaamini utasaidia kufanikisha malengo waliyojiwekea ndani ya umoja wao.

“Tupo kwenye hatua za awali za kuandikisha ushirika na baada ya hapo tunapeleka mambo yetu kwa pamoja LATRA na baadae tutakabidhiwa hati na kuingia nao mkataba kama vile ukataji wa leseni za LATRA na tutapata gawiwo litakalotuwezesha kutekeleza mipango na maono ya ushirika wetu” ameeleza Bw. Constantine.

Aidha, Bw. Constantine amewaasa wamiliki wenzake kujitokeza kwa wingi kujiunga kwenye ushirika ili waweze kujikwamua kiuchumi. “Ushirika huu ni fursa na tunaendelea kuwahamasisha wanachama na bodaboda wote ndani ya Mkoa wa Arusha wajitokeze kwa wingi kujiunga na huu ushirika kwa sababu tutanufaika na kuboresha hali zetu za maisha kwa kufungua miradi mbalimbali tutakayoiendesha wenyewe kwa ushirika wetu” amesema Bw. Constantine.

Bw. Bill Albano, Mwenyekiti Umoja wa Daladala Jiji la Arusha (UWADAJA) amewaasa madereva na wamiliki wa daladala kujiunga kwenye ushirika kwakuwa unamanufaa makubwa kwao na wao kama wamiliki wapo tayari kufanya nao kazi kwa pamoja ili waweze kuinuana kiuchumi na kijamii.  

Mamlaka inaendelea kuwapatia elimu ya uanzishwaji wa vyama vya ushirika kwa madereva na wamiliki wa vyombo vya moto kibiashara kwa kuwa itawasaidia katika kutekeleza majukumu yao kwa uweledi na ufanisi, itakuwa rahisi kwa Mamlaka kuwaratibu wakiwa katika majukumu yao, itawasaidia kukua kiuchumi na kuweza kusaidiana wao wenyewe na kikubwa zaidi itaongeza heshima ya kazi wanayoifanya.

Vilevile vyama vya ushirika vitawawezesha kupata fursa ya kujiwekea taratibu za utoaji huduma za usafirishaji, kupata mitaji kwa ajili ya kuboresha au kuongeza huduma pamoja na kupata elimu ya mara kwa mara ya biashara, usalama barabarani na masuala mengine na kukopeshana vitendea kazi.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo