Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MADEREVA PIKIPIKI NA BAJAJI WATAKIWA KUFUATA SHERIA
Imewekwa: 12 Feb, 2025
MADEREVA PIKIPIKI NA BAJAJI WATAKIWA KUFUATA SHERIA

Madereva pikipiki za magurudumu mawili (Bodaboda), Pikipiki za magurudumu matatu (Bajaji) na Pikipiki za kubeba mizigo (Maguta) Wilaya ya Korogwe wametakiwa kufuata Sheria za usafiri ardhini nchini ili kufanikisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Hayo yameelezwa na Bi. Gloria Sanga, Afisa Tarafa Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga aliyemuwakilisha Mhe. William Mwakilema, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe kwenye kikao kazi cha kutoa elimu ya kazi na majukumu ya LATRA kwa wadau wa usafirishaji kilichoendeshwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Wilaya ya Korogwe, Mkoani Tanga Februari 05, 2025.

“Ni jukumu lenu kuzingatia Kanuni na kufuata Taratibu za usafirishaji hususan kuwa na leseni za LATRA pamoja na kutojihusisha kwenye vitendo vihalifu kwakuwa mmepewa dhamana ya kubeba maisha ya watu na mkisababisha ajali zitagharimu maisha ya binadamu,” amesema Bi. Sanga.

Naye Bw. Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA amewataka wasafirishaji kuzingatia elimu waliyoipata ili kuongeza uelewa katika utekelezaji wa Kanuni, Sheria na Taratibu za leseni za usafirishaji.

 “Mamlaka imewapatia elimu hii ili kuongeza mwamko wa ukataji leseni za LATRA na mnapaswa kufuata Sheria za nchi ili kuepuka athari za kutofuata Sheria. Na Serikali imepitisha Kanuni za Usafirishaji za mwaka 2024 ambapo imeruhusu ushirika kwa wasafirishaji unaolenga kuongeza wigo wa ukataji leseni za LATRA na asilimia ishirini ya mapato mtakayopeleka LATRA yatarudishwa kwenye ushirika wenu,” amesema Pazzy.

Kwa upande wake, ASP Richard Muwe, Kaimu Mkuu wa Usalama Barabarani – Korogwe amewasihi wadau hao kujiunga na Vyama vya ushirika (SACCOS). “Mjitokeze kwa wingi kupata elimu, mshikamane wala msirudi nyuma na mchangamkie fursa hii ya kuunda Vyama vya Ushirika itakayoleta tija katika kujikwamua kiuchumi pia niwakumbushe kuwa jukumu la ulinzi na usalama kwa wilaya yetu ni jukumu letu sote,” amesisitiza ASP Muwe.  

Bw. Masoud Mohamed, Afisa Mfawidhi ofisi ya LATRA Wilaya ya Korogwe amesema ofisi hiyo imesogeza karibu huduma za usafiri ardhini kwa wasafirishaji na wadau kwa jumla ukizingatia Korogwe ni sehemu rahisi kufikika kutoka Wilaya zingine kama Lushoto na Handeni  na hivyo imerahisisha udhibiti wa huduma za usafiri na usafirishaji.

Wakati huohuo, Bw. Alinani Ateli, ameishukuru LATRA kuwapatia elimu ya kuunda vyama vya ushirika, “Umoja wa Bajaji Wilaya ya Korogwe, ni wakataji wazuri sana wa leseni za LATRA, na nawashauri wenzangu wa pikipiki za magurudumu mawili pamoja na Pikipiki za kubeba mizigo maguta nao waingie kwenye ukataji wa leseni hizi ili tunapounda Chama chetu cha Ushirika basi kikawe ni Chama chenye nguvu na manufaa kwetu sote,” amesisitiza Bw. Ateli.

Kikao kazi hicho kilihudhuriwa na wadau wa usafirishaji wapatao 100 wakiwemo madereva na wamiliki wa pikipiki za magurudumu mawili (Bodaboda), magurudumu matatu (Bajaji) na Pikpiki za kubeba mizigo (Maguta) pamoja na viongozi mbalimbali kutoka Wilaya ya Korogwe na Maafisa wa LATRA.

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo