Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MADEREVA WAASWA KUTOTUMIA VILEVI
Imewekwa: 15 Dec, 2025
MADEREVA WAASWA KUTOTUMIA VILEVI

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imewaasa madereva wa vyombo vya moto kibiashara kutotumia vilevi ili kuepusha ajali zinazogharimu maisha ya abiria na mali zao.  

Amebainisha hayo Bw. Patel Ngereza, Afisa Mfawidhi LATRA Mkoa wa Dar es Salaam Desemba 11, 2025 kwenye kipindi cha malumbano ya hoja kilichofanyika katika kituo cha habari cha ITV.

“Kanuni za uthibitishaji wa madereva na usajili wa wahudumu wa vyombo vinavyodibitiwa na LATRA za mwaka 2020 zinamtaka dereva asitumie kilevi chochote pindi anapoendesha basi ama chombo cha moto kibiashara na kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mamlaka inafanya kaguzi mbalimbali za kushtukiza kukagua kiwango cha kilevi kwa madereva kabla hawajaanza safari. Wapo baadhi ya madereva wasiojitambua wanatumia vilevi na Mamlaka inaendelea kutoa elimu kwa madereva hao namna bora ya kutekeleza majukumu yao kwakuwa uhai wa abiria upo mikononi mwao,” amesema Bw. Ngereza.

Vilevile amesema, Mamlaka inatumia mifumo mbalimbali ya kiudhibiti ikiwemo Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) https://vts.latra.go.tz/ unaofuatilia mwenendo wa dereva anapokuwa safarini, Mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS) https://pis.latra.go.tz/ unaomwezesha abiria kufahamu mwendo na mahali basi lilipo na Mfumo tumizi wa LATRA App unaowezesha kufahamu viwango vya nauli, uhai wa leseni pamoja na makosa ya chombo husika,” amesema Bw. Ngereza.

Bw. Majura Kafumu, Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva wa Mabasi Tanzania (UWAMATA) amesema chama hicho kinaendelea kuwapatia elimu madereva ili kuhakikisha suala la usalama linazingatiwa huku wakitekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria zilizopo.      

Bw. Juma Libenanga, Mkurugenzi kanda ya Mashariki na Pwani Shirika la Kutetea Haki za Abiria (SHIKUHA) amesema, “Tunashirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa elimu kwa abiria na kuwahimiza kutoa taarifa za uvunjifu wa Sheria, Taratibu na Kanuni za usafiri ardhini wawapo safarini ukizingatia ulevi wa madereva unachangia ajali ambazo zinaepukika,” amesema Bw. Libenanga.   

Kifungu cha 5(1)(e) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhiti Usafiri Ardhini (LATRA) Sura ya 413 kimeipa LATRA jukumu la kusajili wahudumu na kuthibitisha madereva wa vyombo vya moto kibiashara ili kuhakikisha wanakuwa na sifa, uweledi na wanazingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za usafirishaji kwa lengo la kuwezesha ubora wa huduma za usafiri ardhini nchini.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo