Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MADEREVA WAHIMIZWA KUJITOKEZA ILI KUSAJILIWA NA KUTHIBITISHWA
Imewekwa: 15 Jan, 2023
MADEREVA WAHIMIZWA KUJITOKEZA ILI KUSAJILIWA NA KUTHIBITISHWA

Na Mambwana Jumbe

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) CPA Habibu Suluo amewahimiza madereva wanaoendesha  mabasi yanayosafirisha abiria kwenda mikoani na nje ya nchi kuondoa hofu na kujitokeza kwa wingi ili kusajiliwa na kufanyiwa ithibati.

Akizungumza baada ya kikao cha tathmini ya udhibiti wa usafiri wa abiria kipindi cha mwisho mwaka kilichofanyika katika ofisi za LATRA Dar es Salaam kati ya LATRA na Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) ijumaa Januari 13, 2023, CPA Suluo amesema moja ya faida ya kuwasajini na kuwafanyia ithibati madereva ni kila dereva atawajibishwa kulingana na kosa lake.

“Asilimia kubwa ya ajali zinazotokea barabarani zinatokana na makosa ya kibinadamu, na sisi hatuwajui hawa madereva, hivyo wakisajiliwa itakuwa ni rahisi kumtambua kupitia kifaa kinachounganishwa pamoja na mfumo wa kufuatilia mwenendo wa magari (VTS), kwa hiyo itakuwa rahisi kwa kila mmoja kuwajibishwa kwa kosa lake”, amesema CPA Suluo.

Aidha CPA Suluo amesema LATRA imekubaliana na wadau kuwa si lazima dereva anaposajiliwa afanye na mtihani wa kuthibitishwa, madereva wataruhusiwa kuendesha mabasi wakiwa wamesajiliwa huku wakifuatiliwa mienendo yao ya uendeshaji.

“Tumekubaliana tusiwalazimishe kwanza kufanya mitihani, wanachotakiwa kufanya kwanza ni kuja kujisajili wakiwa na viambata vinavyotakiwa, baada ya kusajiliwa ataruhusiwa kuendelea kuendesha magari, lakini pindi litakapotokea kosa litokanalo na uzembe, leseni yake ya udereva itasimamishwa hadi aje kufanya mtihani, na wenzetu Jeshi la Polisi hawataihuisha leseni bila kuwa na cheti kutoka LATRA”, ameeleza CPA Suluo.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani SACP Ramadhani Ng’anzi amesema, anaamini yote yaliyoazimiwa katika kikao hicho yatafanikishwa kwa wakati ili kuhakikisha kuna huduma ya usafiri iliyo bora.

“Napenda kumshukuru mwenyeji wetu Mkurugenzi Mkuu wa LATRA CPA Habibu Suluo kwa mwaliko wake katika kikao hichi, kimekuwa kikao cha kujenga kwa muda wote tuliokaa, ni matumaini yangu kuwa yote tuliyoazimia yatafanikishwa kwa wakati na tutakuwa na huduma bora ya usafiri nchini”, amesema SACP Ng’anzi.

Katika nafasi nyingine Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi (TABOA) Bw. Issa Nkya amewataka abiria kuzitambua haki zao za msingi na kuzisimamia ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza huku akiwaasa madereva kufuata Sheria za Usalama Barabarani na kuzingatia suala la kusajiliwa na kufanyiwa ithibati.

“Ninawasihi abiria kuhakikisha kuwa nauli anayolipia ipo sawa na nauli iliyoandikwa kwenye tiketi, kiujumla abiria anapaswa kuhakikisha kuwa taarifa zote za msingi zimeandikwa katika tiketi ya kielekroni kwa usahihi ili kujiepusha na changamoto mbalimbali”, amesisitiza  Bw. Nkya.

Vilevile Bw. Nkya ametoa wito kwa madereva wote kuhakikisha wanafuata kikamilifu Sheria na alama za barabarani kadiri ya maelekezo yanayokuwepo, pia kujitokeza kwa wingi kusajiliwa na kuthibitishwa ili waweze kusimamiwa kikamilifu.

Kwa mujibu wa Sheria ya LATRA 5 (1) (e), LATRA imepewa jukumu la kuthibitisha madereva na kuwasajili wahudumu. Mpaka sasa zaidi ya madereva 700 wamejitokeza kwa ajili ya kusajiliwa na kufanyiwa ithibati na karibu robo tatu ya wote waliofanya mtihani wamefaulu na kuthibitishwa.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo