Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MADEREVA WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA LATRA, JESHI LA POLISI
Imewekwa: 07 Dec, 2022
MADEREVA WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA LATRA, JESHI LA POLISI

Na Mambwana Jumbe

Mkuu wa Wilaya ya Rombo Mhe. Kanali Hamis Maiga amewataka madereva wa mabasi ya masafa marefu Mkoa wa Kilimanjaro kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani katika majukumu yao na pia amewataka kuzingatia Sheria na Kanuni za Usalama Barabarabi ili kuepuka ajali zinazogharimu maisha ya wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu wakati wa ukaguzi wa pamoja wa mabasi ya masafa marefu uliofanywa na LATRA, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Jeshi la Polisi pamoja na wadau wengine wa usafirishaji katika Stendi Kuu ya Mabasi ya manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro, Kanali Maiga alisema madereva wakiwa karibu na LATRA na Jeshi la Polisi, itakuwa rahisi katika kutekeleza Sheria za Usalama Barabarani.

Kanali Maiga aliongeza kuwa, ni wajibu wa madereva kuzingatia mwendo ulioidhinishwa na Serikali ili kupunguza na kuondokana na tatizo la ajali ambazo zimekuwa zikiondoa nguvukazi ya Taifa.

“Suala la ajali kipindi cha mwisho wa mwaka katika Mkoa huu wa Kilimanjaro limekuwa ni tatizo kubwa  na tumekuwa tukipoteza wananchi ambao ndio chachu ya kuleta maendeleo katika mkoa wetu na Taifa kwa jumla, hivyo nawasihi madereva kuacha kuendesha mabasi kwa mwendokasi ili kuyalinda maisha ya wananchi kwa mustakabali mzuri wa maisha yao na familia zao,” Kanali Maiga alieleza

Naye Afisa Mfawidhi LATRA Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Paul Nyello alizungumzia mabasi ya hakuna kulalal ambayo yamekuwa yakifanya biashara ya usafirishaji usiku na alisema kuwa LATRA inatoa onyo na inawakumbusha kutekeleza majukumu yao kulingana na leseni walizonazo na vinginevyo Mamlaka itachukua hatua kwa kuwa wanachofanya ni kinyume na taratibu zilizopo.

 “Tunawaasa abiria ambao wamekuwa wakipanda mabasi hayo waache hiyo tabia kwakuwa wanahatarisha maisha yao maana wale madereva hawapumziki wanafika mwisho wa safari na wanageuza jambo ambalo ni hatari kwa maisha yao, tujaribu kuyajali maisha yetu kwanza kabla ya kufikia hatua ya kupanda kwenye hakuna kulala. Watumie vyombo sahihi vilivyothibitishwa na LATRA kwa ajili ya usalama wao na familia zao,”

Akizungumzia suala la mwendokasi, Bw. Nyello alisema, LATRA na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani wamejipanga kuhakikisha kuwa madereva wanaendelea kupata elimu ya usalama barabarani lakini pia ikitokea wanaenda kinyume na Sheria na taratibu zilizopo hawatasita kuchukua hatua kali dhidi yao.

Akizungumzia kipindi cha mwisho wa mwaka, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro ACP Simon Maigwa alisema Mkoa huo upo salama na wanaendelea kudhibiti matukio ya ajali na hiyo ni kutokana na mipango thabiti waliyonayo kwa kushirikiana na LATRA pamoja na vyombo vingine vya usalama hapa nchini

“Natoa rai kwa yeyote anayeingia mkoa wa Kilimanjaro anazingatia Sheria za usalama barabarani. Tutaendelea kufanya ukaguzi wa mabasi tukishirikiana na LATRA ili kuhakikisha kuwa masuala haya ya usalama yanazingatiwa na kufuatwa na madereva wetu ili kuepukana na ajali,” ACP Maigwa alisisitiza.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo