Bw. Andrew Magombana, Mkurugenzi Msaidizi Usafiri kwa njia ya Barabara Wizara ya Uchukuzi amesema rasimu za Kanuni za Usimamizi wa Madhara ya Uchovu kwa Madereva za mwaka 2026 ni nyenzo muhimu ya kuimarisha sekta ya usafirishaji nchini,
Bw. Magombana amesema hayo Januari 8, 2026 katika mkutano wa kupokea maoni ya wadau kuhusu Rasimu za Kanuni za Usimamizi wa Madhara ya Uchovu kwa Madereva za mwaka 2026, ukumbi wa Mikutano Chuo cha Utalii Dar es Salaam.
Akizungumza kwa niaba ya Prof. Godius Kahyarara, Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Bw. Magombana ameeleza kuwa zipo changamoto mbalimbali katika usimamizi wa vyombo vya moto kibiashara zinazoongeza uhitaji wa kuwa na Kanuni hizo muhimu zinazolenga kuwasimamia watoa huduma za usafiri na madereva katika usimamizi wa madhara yanayotokana na uchovu wakati wakiendesha vyombo ambavyo vinadhibitiwa na Mamlaka.
“Changamoto ambazo zimeonekana ni kutokuwepo kwa Kanuni mahsusi za kushughulikia na kufanya udhibiti katika usimamizi wa uchovu wa madereva wa vyombo vya usafiri kwa njia ya barabara, kuwepo kwa ongezeko la ajali mbalimbali zinazosababishwa na uchovu wa madereva hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali imerushusu mabasi ya abiria kufanya kazi saa 24 na kukosekana kwa nyenzo ya kulinda afya za madereva wa usafiri ardhini ili kuhakikisha wanapata muda wa kutosha kupumzika,” amesema Bw. Magombana.
Vilevile amesema, wamiliki wa vyombo vya moto kibiashara wanatakiwa kuandaa mpango wa usimamizi wa madhara ya uchovu kwa lengo la kuimarisha sekta ya usafirishaji.
“Rasimu ya Kanuni hizi zimetoa wajibu kwa madereva na kwa wamiliki wa vyombo katika usimamizi wa madhara ya uchovu ambapo wamiliki wanatakiwa kuandaa mpango wa usimamizi wa madhara ya uchovu na Matarajio ya Serikali ni kwamba, endapo kila mmoja atatimiza kikamilifu wajibu wake kama ilivyoainishwa katika Rasimu ya Kanuni hizi, ubora na usalama wa usafiri wa abiria na mizigo kwa njia ya barabara utaongezeka,” ameeleza Bw. Magombana.
Kwa upande wake CPA, Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA amesema kuwa, uchovu wa madereva ni miongoni mwa sababu kubwa zinazosababisha ajali za barabarani ambazo zinagharimu maisha ya watu na mali zao.
“Dereva anapochoka na kuendelea kuendesha gari, hatari ya ajali huwa kubwa na ikitokea tunapoteza uhai wa watu, wengine wanapata ulemavu na taifa linaingia gharama kubwa za matibabu na kupoteza nguvu kazi. Kanuni hizi zinalenga kuweka mifumo madhubuti ya kudhibiti muda wa kazi na mapumziko ya madereva, usimamizi wa ratiba za safari, pamoja na wajibu wa waajiri na wamiliki wa vyombo vya usafiri katika kuhakikisha usalama unazingatiwa,” amesema CPA, Dkt. Suluo.
Vilevile CPA, Dkt. Suluo amesema, Serikali imeona umuhimu wa kuchukua hatua mapema ili kuzuia madhara makubwa yanayotokana na uchovu wa madreva, hususan katika usafiri wa masafa marefu na usafirishaji wa mizigo na kulinda mitaji ya wawekezaji, kulinda afya na usalama wa madereva wao na hasa kulinda uhai wa wananchi .
Rasimu za Kanuni za Usimamizi wa Madhara ya Uchovu kwa Madereva za mwaka 2026, zimeandaliwa na Wizara ya Uchukuzi kwa kushirikiana na LATRA na zinapatikana kwenye tovuti ya LATRA www.latra.go.tz ambapo wadau wanaweza kuwasilisha maoni yao kwa maandishi kupitia baruapepe group.maoni@latra.go.tz hadi tarehe 22 Januari 2026 ikiwa ni siku 14 baada ya mkutano huo.

