Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MAGOMBANA: MAONI YENU NI MUHIMU KATIKA KUBORESHA KANUNI ZA LATRA
Imewekwa: 15 May, 2023
MAGOMBANA: MAONI YENU NI MUHIMU KATIKA KUBORESHA KANUNI ZA LATRA

Wadau wa Sekta ya Usafiri Ardhini Mkoani Kilimanjaro wamesisitizwa kutoa maoni yao kuhusu Rasimu za Kanuni Mpya za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kuwa maoni hayo ndio chachu ya kuboresha kanuni hizo

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Usafiri kwa Njia ya Barabara kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) Bw, Andrew Magombana ambaye alimuwakilisha Katibu Mkuu Gabriel Migiro kwenye Mkutano wa Kupokea Maoni ya Wadau Kuhusu Rasimu za Kanuni Mpya za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini uliofanyika Mei 15, 2023 Mkoani Kilimajaro.

“Mkutano huu ni sehemu muhimu katika mchakato wa kuandaa Kanuni hizi. Nitumie fursa hii kuwaomba muwe huru kujadili Kanuni hizi zinazopendekezwa na kutoa maoni yenu yatakayoboresha utekelezaji wa Kanuni hizo ili kuleta tija katika sekta ya usafirishaji ambayo ina mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa letu," amesema Magombana.

Aidha, Magombana amesema kuwa wakati LATRA inaendelea kutekeleza majukumu yake ya udhibiti, imekuwa ikikumbana na changamoto mbalimbali kama vile kutokuwepo kwa Kanuni mahsusi za kushughulikia usafirishaji wa bidhaa hatarishi kwa upande wa barabara kama ilivyo kwenye usafiri wa Majini na njia ya Reli, kuwepo na baadhi ya wadau ambao wanapaswa kudhibitiwa lakini hawadhibitiwi hivyo kuleta athari mbalimbali katika tasnia zinazodhibitiwa; kutokuwepo kwa Kanuni mahsusi zitakazoonesha utaratibu wa huduma za kimtandao kama vile Tiketi Mtandao na Mfumo wa Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Vyombo vya Usafirishaji, na kuendelea kuwepo na kutumika kwa  Kanuni ya iliyokuwa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Nchi Kavu na Majini (SUMATRA).

“Kwa kuzingatia hayo, Wizara kwa kushirikiana LATRA tukaandaa rasimu hizi 8 ili kupata suluhu ya changamoto hizo.Tumeitisha vikao vya wadau ili kupata maoni yenu kwa kuwa ninyi ndio wadau wakuu katika hili na Kanuni hizi ni zenu,” amesisitiza Magombana

Naye Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara kutoka LATRA Bw. Johansen Kahatano amesema LATRA imeanzishwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Adhini, Sura ya 413 na imepewa jukumu la kudhibiti huduma za usafiri wa ardhini. Aidha, katika Sheria hiyo na Sheria ya Leseni za Usafirishaji, Sura ya 317, Waziri amepewa Mamlaka ya kutengeneza Kanuni mbalimbali zitakazowezesha Sheria hizo kutekelezwa ipasavyo.

Naye Afisa Sheria Mwandamizi kutoka LATRA Bi. Mwadawa Sultan amesema ushirikishwaji wa wadau ni sehemu muhimu ili kupata maoni yatakayoboresha utendaji kazi wa Mamlaka pamoja na sekta nzima ya Usafiri Ardhini hapa nchini, “Zipo baadhi ya Kanuni ambazo bado zinasomeka kwa jina la Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Nchi (SUMATRA) kwa hiyo mchakato huu wa utengenezaji wa rasimu hizi ukikamilika, zitafutwa ili ziweze kusomeka kwa jina la LATRA kwa sababu SUMATRA ilivunjwa.”

Aidha, Bi. Mwadawa amezitaja Rasimu za Kanuni hizo nane (8) kuwa ni; Kanuni za Mamlaka Udhibiti Usafiri Ardhini za Uwezeshaji wa Huduma za Usafiri za Mwaka 2023 zinazolenga kuwadhibiti watoa huduma, bidhaa au vifaa vinavyowawezesha Watoa Huduma zinazodhibitiwa kufanya shughuli zinazodhibitiwa. Mfano Mawakala na wasambazaji wa vifaa vya ufuatiliaji wa mwenendo wa vyombo vinavyodhibitiwa., Kanuni za Mamlaka Udhibiti Usafiri Ardhini za Ukaguzi wa Lazima wa Vyombo vinavyotoa Huduma za Usafirishaji Kibiashara za Mwaka 2023; zinazolenga kutekeleza kifungu cha 5(1) (f) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura ya 413.

Vilevile amesema Kanuni nyingine ni; Kanuni za Mamlaka Udhibiti Usafiri Ardhini za Ufifilishaji wa Makosa  za Mwaka 2023 zinazolenga kufuata utaratibu uliowekwa na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali kupitia Sheria ya Taifa ya Mashtaka Sura ya 430 katika kufifilisha makosa, Kanuni za Leseni za Usafirishaji za Vyombo Vinavyosafirisha Bidhaa Hatarishi za Mwaka 2023 ambapo kumeonekana haja ya kuwa na Kanuni mahsusi za Usafirishaji wa Bidhaa Hatarishi kama ilivyo kwa upande wa usafiri wa majini na reli. Vilevile ni suala la kimataifa katika kulinda afya na mazingira dhidi ya athari za bidhaa hatarishi zinazo safirishwa ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu.

Bi Mwadawa amezitaja Kanuni nyingine ambazo ni; Kanuni za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini za Vigezo na Masharti ya Kutoa Huduma zinazodhibitiwa za Mwaka 2023; ambazo zimerithiwa kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) hivyo lengo la sasa ni kuzihuishwa ziwe rasmi chini ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na  Kanuni za Mamlaka za Udhibiti Usafiri Ardhini  za Utaratibu wa Kushughulikia Malalamiko za Mwaka 2023 ambazo  zimerithiwa kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) hivyo lengo la sasa ni kuzihuishwa ziwe rasmi chini ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA).

“ Kanuni nyingine tunazokusanya maoni ya wadau ni Kanuni za Mamlaka za Udhibiti Usafiri Ardhini  za Matumizi ya Tiketi Mtandao za Mwaka 2023 zinazolenga kuweka utaratibu wa kuwatambua kwa kuwasajiri na kuweka masharti juu ya kuendesha mfumo wa tiketi mtandao bila kupelekea usumbufu wa Watoa Huduma pamoja na Kanuni za Mamlaka za Udhibiti Usafiri Ardhini za Mfumo wa Ufuatiliaji wa Mwenendo wa vyombo vya Usafirishaji Kibiashara zinazolenga kudhibiti wasambazaji wa vifaa vinavyotuma taarifa kwenye Mfumo wa Ufuatiliaji Mwenendo wa Vyombo na kuweka vigezo na masharti ya kufanya usambazaji huo," ameeleza Bi. Mwadawa.

Mei 08, 2023 Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) alitoa Taarifa kwa Umma kuhusu Mikutano ya Kupokea Maoni ya Wadau Kuhusu Rasimu za Kanuni Mpya za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini kwa tarehe 15, 17 na 19 inayofanyika Kanda ya Kati, Kanda ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Ziwa pamoja na Kanda ya Mashariki.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo