Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MAJARIBIO TRENI YA SERENGETI YAKAMILIKA
Imewekwa: 29 Dec, 2024
MAJARIBIO TRENI YA SERENGETI YAKAMILIKA

Seti ya nne kati ya 10 za treni ya umeme aina ya EMU maarufu kama mchongoko iliyopewa jina la Serengeti imefanyiwa majaribio ya mwisho kabla ya kupatiwa ithibati na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa ajili ya kuanza kutoa huduma ya usafiri kwenye reli ya kisasa (SGR).

Majaribio hayo yamefanyika tarehe 27 na 28 Desemba, 2024 kuanzia Stesheni ya Pugu jijini Dar es Salaam hadi Stesheni ya Dkt. Samia Suluhu Hassan jijini Dodoma yakihusisha wataalam wa LATRA, Shirika la Reli Tanzania (TRC) pamoja na kampuni ya Hyundai Rotem ya Korea Kusini ambayo ni mtengenezaji wa treni hizo.

Akizungumza baada ya majaribio hayo, Mha. Moses Nyoni, Kaimu Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Reli LATRA amesema katika majaribio hayo, wamekagua maeneo mbalimbali ikiwemo usalama wa uendeshaji, mifumo ya umeme pamoja na maeneo mengine ya kiufundi.

“Tumekagua treni hii kwa lengo la kuangalia mwenendo wa uendeshaji pamoja na ubora wa mifumo yake, pia tumeangalia namna madereva wanavyoendesha treni hizi kwa viwango vilivyowekwa kwa mujibu wa taratibu zilizopo. Tunafanya hivi ili kuhakikisha usalama unazingatiwa na hatimaye tuwe na usafiri usio na chembe ya shaka kiusalama,” ameeleza Mha. Nyoni.

Akitoa tathmini baada ya majaribio hayo, Mha. Nyoni amesema kuwa, LATRA imeridhishwa na mwenendo wa treni hiyo kwa maana kwamba vigezo vya msingi vilivyotolewa na TRC, vimezingatiwa kwa kiasi kikubwa na mkandarasi na kuna maboresho makubwa wameyaona kuanzia kwenye muundo na jinsi mifumo yote inavyofanya kazi.

Kwa upande wake, Edga  Bakuza, Mhandisi wa mitambo mwandamizi TRC ameeleza majaribio hayo yamefanyika kwa ufanisi na wanategemea treni hiyo kuanza safari zake hivi karibuni na hivyo kufanya jumla ya treni aina ya EMU kuwa nne (04) ambapo tatu za mwanzo zinazoendelea na kazi ya usafirishaji abiria ni  treni ya Nyerere, Magufuli na Samia.

Wananchi nao wamepongeza jitihada za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uwekezaji mkubwa alioufanya na kuwezesha fursa za usafiri wa reli ulio wa kisasa na hivyo kurahisisha shughuli zao za kila siku.

Treni ya Serengeti inaongeza idadi ya safari za treni zitakazoleta tija kwa kuchochea fursa za kufanya biashara kwa wakati na hivyo kuongeza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Serikali kwa jumla.

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo