Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MBEYA NA RUKWA WAPATIWA ELIMU YA TIKETI MTANDAO
Imewekwa: 20 Nov, 2022
MBEYA NA RUKWA WAPATIWA ELIMU YA TIKETI MTANDAO

Na Mambwana Jumbe

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani imeendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi ya Mfumo wa Tiketi Mtandao kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa na Mbeya.

Elimu hiyo imetolewa na Afisa Mfawidhi Rukwa Bw. Athumani Nyiga, Afisa Mfawidhi Mbeya Bw. Omary Saleh pamoja na Mrakibu wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Rukwa SP Wenceslaus Gumha ambapo kwa nyakati tofauti wamewasihi wananchi na wasafiri wa mikoa hiyo kuendelea kukata tiketi kwa njia ya mtandao kwa kuwa mfumo huo ni rahisi na salama.

Bw. Saleh alipofanya ukaguzi wa tiketi mtandao hivi karibuni alisema kuwa mwamko wa abiria kwenye matumizi ya mfumo wa tiketi mtandao kwa Mkoa wa Mbeya ni mkubwa na kwa magari yanayokaguliwa abiria ambaye hana tiketi ya mashine ya kielektroni basi anayo ile ya kwenye simu jambo ambalo linaonesha kuwa elimu ya matumizi ya mfumo huo imewafikia wadau.

“Sisi kama Mamlaka pamoja na Jeshi la Polisi na wadau wengine tutaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi ya mfumo huu ili kila mmoja wetu aelewe faida zake,” ameeleza Bw. Saleh

Akielezea faida za mfumo huo, Bw. Saleh amesema mfumo wa Tiketi Mtandao unamwezesha abiria kukata tiketi kutokea mahali popote na kuepukana na adha za wapiga debe na kwa upande wa wasafirishaji wanaweza kudhibiti mauzo ya tiketi kwa kuwa mfumo unawawezesha kuona mauzo yote yanayofanyika kupitia simu za mkononi na vilevile Serikali inapata mapato yake na hivyo amewasihi wananchi kuendelea kujifunza na kutumia tiketi mtandao

Naye Bw. Nyiga alisema, “tiketi hizi za mtandao zinamwezesha abiria kuchagua kiti anachokitaka na basi analolitaka ambapo kwa zamani suala kama hili lilikuwa na changamoto na abiria walikuwa wanagombaniwa lakini kwa sasa abiria akishakata tiketi yake anaelekea moja kwa moja kwenye gari alilokata na kukaa kwenye kiti alichokichagua na kusafiri kwa amani, kwakweli mfumo huu unawaondolea bugudha wananchi’”, alifafanua

Kwa upande wa SP Gumha amewasihi wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga Mkoani Rukwa kutumia mfumo wa Tiketi Mtandao ili kuepukana na usumbufu kwakuwa wanaweza kukata tiketi hizo sehemu yoyote na wakati wowote

Vilevile amesema, LATRA na Jeshi la Polisi wataendelea kushirikiana ili kuhakikisha kwamba wananchi wote na wasafirishaji wanapata uelewa wa matumizi ya mfumo wa Tiketi Mtandao kwa kuwa mfumo huo una faida kubwa kwa wananchi, mmiliki na Serikali kwa jumla.

Akizungumzia matumizi ya tiketi hizo Bi. Prisca Ngoli ambaye ni abiria aliipongeza LATRA kwa kutengeneza mfumo rafiki ambao umesaidia kuondoa usumbufu uliokuwepo awali wa kutumia gharama za usafiri kwenda kukata tiketi kwenye vituo vya mabasi.

“Kwa kweli mfumo huu ni mkombozi sana kwetu nakumbuka tulipokuwa tunatumia ule mfumo wa zamani tulikuwa tunakatiwa tiketi moja watu wawili yaani tukiingia kwenye basi ni vurugu maana kila mmoja anataka kukaa kwenye kiti alichokata tiketi lakini kwa mfumo huu wa sasa purukushani hizo hakuna, abiria unakata tiketi kwenye simu yako na ukija unakuta kiti chako kiko wazi,” alieleza Bi. Prisca

Kwa upande wake Bw. Abbas Mwambenja amesema kuwa mfumo wa Tiketi Mtandao umesaidia kutozwa nauli halali zilizotolewa na kuidhinishwa na LATRA tofauti na mfumo wa zamani ambapo wananchi walikuwa wanatozwa nauli kiholela.

“Mimi ninafurahia sana mfumo huu, Wakala kanikatia tiketi nikapata ujumbe mfupi kwenye simu yangu na haikuchukua muda mrefu nikapatiwa risiti ya kwenye mashine na hii inasaidia maana hata tiketi ikipotea, nitaonesha hii ya kwenye simu yangu, kwa kweli huduma hii nimeipenda sana” amefafanua Bw. Mwambenja

Naye Bw. Uswege Mwandambo, dereva wa basi la Kampuni ya New Force linalotoka Mbeya kwenda Dar es Salaam alisema kuwa kwa sasa abiria wengi wamekuwa na uelewa mkubwa wa kutumia tiketi mtandao tofauti na siku za mwanzoni mfumo ulipoanza kutumika.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo