Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MHA. KISAKA: KUWENI HURU KUTOA MAONI YENU
Imewekwa: 16 May, 2023
MHA. KISAKA: KUWENI HURU KUTOA MAONI YENU

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) imewataka wadau wa Usafiri Ardhini kuwa huru na kujitokeza kwa wingi ili kutoa maoni katika Rasimu za Kanuni za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) za mwaka 2023 ambazo zinajadiliwa katika mikutano ya wadau wa Usafiri Ardhini inayoendeshwa na Wizara hiyo.

Hayo yamesemwa na Mhandisi Aroni Kisaka, Mkurugenzi wa Huduma za Usafiri kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Uchukuzi) alipokuwa akifungua Mkutano wa wadau wa Usafiri Ardhini uliofanyika Kanda ya Kati (Mkoa wa Dodoma), akimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Uchukuzi) Bw. Gabriel Migire.

Mha. Kisaka amewaambia wadau hao kuwa, wanapaswa kuwa huru na kutumia nafasi hiyo vizuri kwani mchango wao ndio utakaosaidia kupatikana Kanuni bora, huku akiwahimiza kutumia njia zote za kutoa maoni.

“Nawaomba muwe huru mnapotoa maoni yenu na tumieni muda wenu vizuri, na siku 14 ambazo tumewapatia tumieni vizuri kwa kupitia vizuri Rasimu hizi, ili hata pale ambapo utakuwa umesahau kutoa maoni kwa siku ya leo basi uweze kutuma maoni yako katika anwani mtakazopatiwa” amesema Mha. Kisaka.

Aidha, Mha. Kisaka amesema zipo sababu nyingi zilizopelekea kuwepo kwa Rasimu hizi, ikiwemo kuwepo kwa watoa huduma ambao wanapaswa kudhibitiwa na Mamlaka lakini hawadhibitiwi kutokana na kukosekana kwa kanuni.

“Kwa kipindi kilichopita, Mamlaka imepitia changamoto mbalimbali za kiudhibiti kama vile kukosekana kwa kanuni za kusimamia usafirishaji wa bidhaa hatarishi, kuwepo kwa watoa huduma ambao wanapaswa kudhibitiwa lakini hawadhibitiwi kutokana na kukosekana kwa kanuni mahsusi, hivyo umuhimu wa kuwa na Kanuni hizi unajidhihirisha” ameongeza Mha. Kisaka.

Kwa upande wake CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA amesema LATRA inafanya majukumu yake kwa mujibu wa Sheria kupitia Kanuni mbalimbali huku akiahidi ushirikiano baina ya LATRA na wadau wote wa Usafiri Ardhini.

“LATRA tunafanya kazi kwa mujibu wa Sheria ya LATRA Sura ya 413 pamoja na Sheria nyingine za Kisekta kama Sheria ya Reli ya mwaka 2017, kupitia Kanuni mbalimbali tunaweza kusimamia Sheria hizi ili huduma zitolewe kwa ufanisi zaidi, LATRA tutaendelea kutekeleza majukumu yetu kwa uweledi na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu zote zilizopo” amesema CPA Suluo.

Kwa upande wake Bw. Raymond Samson, mjumbe wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) amewasihi wadau wengine kujitokeza kwa wingi ili kutimiza haki yao ya Kikatiba.

“ Kutokana na Mkutano huu, matumaini yangu ni kuwa kutakuwa na dira nzuri katika sekta ya usafirishaji, hii ni kama maoni ambayo wadau tumeyatoa yatachukuliwa na kufanyiwa kazi, hivyo niwasihi wadau wenginge kwenye kanda zingine ambazo mikutano hii itafanyika wajitokeze ili watimize haki yao ya Kikatiba” amesema Bw. Samson.

Mikutano hii ya wadau wa Usafiri Ardhini kujadili Rasimu ya Kanuni mpya za LATRA inafanyika katika Kanda ya Kati, Kanda ya Kusini, Kanda ya Ziwa, Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Mashariki.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo