Mkurugenzi Msaidizi wa Usafiri kwa Njia ya Barabara kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) Bw. Andrew Magombana amewaambia wadau wa sekta ya usafiri ardhini mkoa wa Dar es Salaam kuwa, maoni wanayotoa yatasaidia kuboresha huduma za sekta ya usafiri ardhini nchini.
Magombana ameeleza hayo alipofungua Mkutano wa Kupokea Maoni ya Wadau Kuhusu Rasimu za Kanuni Mpya nane (08) za LATRA uliofanyika Mei 19, 2023 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Dar es Salaam, akimuwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Uchukuzi) Bw. Gabriel Migire.
“Wizara kwa kushirikiana na LATRA tumeandaa hizi kanuni na kuzisambaza kwenu wadau wetu kwa njia mbalimbali ikiwemo tovuti na mitandao ya kijamii ili muweze kuzisoma na kutoa maoni yenu ambayo yatajumuishwa na maoni ya wadau wengine ili tuweze kupata kanuni zilizo bora ambazo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha sekta nzima ya usafiri ardhini pamoja na utendaji kazi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA),” amesema Magombana.
Vilevile amesema, Kanuni bora ni zile zinazotengenezwa kutokana na maoni ya wadau, ndio maana Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) baada ya kupata rasimu ikaitisha vikao na wadau wa sekta ya usafiri ardhini ili kwa pamoja wapate maoni yatakayoiwezesha Serikali kuboresha huduma na uendeshaji wa sekta hiyo nchini.
Naye Mkurugenzi Mkuu LATRA, CPA. Habibu Suluo amesema “Zipo baadhi ya Kanuni ambazo bado zinasomeka kwa jina la Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) ambayo ilifutwa, kwa hiyo kupitia mchakato huu wa utengenezaji wa rasimu hizi ukikamilika, kanuni hizo zitafutwa ili ziweze kusomeka kwa jina la LATRA.”
Aidha, CPA Suluo amezitaja Kanuni hizo 08 kuwa ni Kanuni za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini za Ukaguzi wa Lazima wa Vyombo vya Usafirishaji Kibiashara za Mwaka 2023, Kanuni za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini za Utaratibu wa Kushughulikia Malalamiko za Mwaka 2023, Kanuni za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini za Vigezo za Masharti za Kutoa Huduma Zinazodhibitiwa za Mwaka 2023 na Kanuni za (Magari Ya Kubeba Bidhaa Hatarishi) za Sheria ya Leseni za Usafirishaji za Mwaka 2023
Vilevile amezitaja Kanuni nyingine kuwa ni Kanuni za Kufifilisha Makosa za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini za Mwaka 2023, Kanuni za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini za Uwezeshaji wa Watoa Huduma za Usafiri za Mwaka 2023, Kanuni ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini za Matumizi ya Tiketi Mtandao za Mwaka 2023 pamoja na Kanuni za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini za Matumizi ya Mfumo wa Ufuatiliaji Mwenendo wa Vyombo vya Usafiri za Mwaka 2023
“Kwa wadau ambao wameshindwa kufika kwenye mikutano hii tuliyoifanya kwa sababu mbalimbali, wanayo nafasi ya kuwasilisha maoni yao kwa maandishi kupitia baruapepe ya group.maoni@latra.go.tz mpaka tarehe 26 Mei, 2023,” amesisitiza CPA Suluo.
Mei 08, 2023 Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) alitoa Taarifa kwa Umma kuhusu Mikutano ya Kupokea Maoni ya Wadau Kuhusu Rasimu za Kanuni Mpya za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini kwa tarehe 15, 17 na 19 iliyofanyika Kanda ya Kati, Kanda ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Ziwa pamoja na Kanda ya Mashariki.