Mkurugenzi Msaidizi wa Usafiri kwa Njia ya Barabara kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) Bw. Andrew Magombana, amesema Rasimu za Kanuni Mpya nane (08) za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) zimelenga kumlinda msafirishaji ambaye anatoa huduma kwa ufanisi pamoja na kuhakikisha mwananchi anapata huduma huduma za usafiri ardhini zilizo bora na salama,
Magombana ambaye alimuwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) Gabriel Migire, amebainisha hayo alipofungua Mkutano wa Kupokea Maoni ya Wadau kutoka Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) Kuhusu Rasimu za Kanuni Mpya nane (08) za LATRA uliofanyika Mei 26, 2023 katika ofisi ya LATRA Mkoa wa Dar es Salaam.
Vilevile amesema kuwa, uandaaji wa Kanuni hizo umechagizwa na changamoto mbalimbali zilizoikuta LATRA kama vile kutokuwepo kwa Kanuni mahsusi za kushughulikia usafirishaji wa bidhaa hatarishi kwa upande wa barabara, kutokuwepo kwa Kanuni mahsusi zitakazoonesha utaratibu wa huduma za kimtandao kama vile Tiketi Mtandao na Mfumo wa Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Magari (VTS) pamoja na kuendelea kuwepo na kutumika kwa Kanuni ya iliyokuwa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Nchi Kavu na Majini (SUMATRA).
“Tunaamini Kanuni hizi zinaenda kuboresha utendaji wa LATRA pamoja na kuifanya Sekta hii ya Usafiri Ardhini hapa nchini kuendeshwa kitaaluma na hivyo kuongeza manufaa na tija kwa wasafirishaji pamoja na wananchi kwa jumla,” amefafanua Magombana.
Aidha, Magombana ameeleza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasisitiza katika kusaidia wawekezaji na wananchi, hivyo amewasihi wadau kutoka TABOA kutoa maoni yao ambayo yataunganishwa na ya wadau wengine ili kupata Kanuni zilizo bora na zenye manufaa kwa wote.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu LATRA CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara kutoka LATRA Bw. Johansen Kahatano amesema LATRA ipo kwa ajili ya kumlinda mtoa huduma za Usafiri Ardhini pamoja na mwananchi ambaye ndiye mtumiaji wa huduma hizo, hivyo TABOA kama mtoa huduma awe huru kutoa maoni ili kufikia malengo yaliyowekwa.
LATRA imekutana na TABOA ambao walishindwa kuhudhuria na kutoa maoni yao kwenye kikao cha Kanda ya Mashariki kilichofanyika Mei 19, 2023 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Dar es Salaam.
Mei 08, 2023 Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) Gabriel Migire alitoa Taarifa kwa Umma kuhusu Mikutano ya Kupokea Maoni ya Wadau Kuhusu Rasimu za Kanuni Mpya za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini iliyofanyika Kanda ya Kati, Kanda ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Ziwa pamoja na Kanda ya Mashariki.