Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MHA. MBAWALA: MAKOSA YA KIBINADAMU CHANZO CHA AJALI ZA TRENI DUNIANI KOTE
Imewekwa: 29 May, 2024
MHA. MBAWALA: MAKOSA YA KIBINADAMU CHANZO CHA AJALI ZA TRENI DUNIANI KOTE

Mha. Hanya Mbawala, Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Reli kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amesema kuwa, chanzo cha ajali nyingi za treni duniani kote husababishwa na makosa ya kibinadamu ambayo hufanywa kwa kukusudiwa ama kwa kutokukusudiwa na wafanyakazi mahsusi wa reli (Safety Critical workers).

Mha. Mbawala amebainisha hayo wakati akitoa mafunzo kuhusu makosa ya kibinadamu kwa wafanyakazi mahsusi wa reli kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC) kituo cha Tanga katika mafunzo ya siku moja yaliyoandaliwa na LATRA, Mei 28, 2024.

Aidha, Mha. Mbawala amewaeleza wafanyakazi hao umuhimu wa kuepuka makosa ya kibinadamu kwa sababu nchi hutumia gharama kubwa kununua treni na kujenga miundombinu ya reli, hii itasaidia kupunguza hasara kwa nchini ikiwemo ajali za treni ambazo huharibu miundombinu ya reli na treni yenyewe.

“Mafunzo haya yatasaidia sana katika kuondoa makosa ya kibinadamu miongoni mwenu kwani makosa hayo husababisha hasara nyingi na kubwa kwa taifa ikiwemo ajali za treni ambazo huharibu miundombinu ya reli na treni yenyewe lakini pia kuepuka kupata harasa za mali na hata kupoteza maisha kwa abiria wanaotumia vyombo hivyo,” amesema Mha. Mbawala.

Vilevile, ameeleza matarajio ya Mamlaka baada ya mafunzo hayo kuwa ni pamoja na kupunguza makosa ya kibinadamu kama kutotengeneza njia ya treni kwa usahihi na kutofikisha treni ikiwa salama, “tunaamini kuwa wafanyakazi hawa watakua wamezingatia mafunzo tuliyowapatia katika semina hii na sasa hivi tunaamini kabisa makosa ya kibinadamu yatapungua kwa upande wa wafanyakazi hawa, na hii itaboresha huduma za treni nchini na kukuza sekta ya Usafiri Ardhini.”

Naye Bw. Rolence Semanini, Meneja wa Reli TRC Kanda ya Tanga amesema, “niwashukuru LATRA kwa kutupatia elimu hii nzuri kwani wametuelekeza mambo ambayo ni msingi mkuu wa usalama wa reli na mambo hayo tunakutana nayo kila iitwapo leo tunapokuwa tukitekeleza majukumu yetu, lakini pia mafunzo haya yameakisi kwa kiasi kikubwa sana utendaji kazi wetu kwa sababu yamegusa idara zote muhimu za uendeshaji wa reli kuanzia utawala hadi watendaji ndani ya treni wakiwemo waongozaji treni na madereva wa treni.”

Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru LATRA kwa kuwapatia mafunzo hayo kwani  yamewapatia mwanga na kuwafanya wawe tayari zaidi kuitumikia sekta ya reli na taifa kwa jumla ili kuleta maendeleo ya pamoja katika sekta ya usafiri wa reli nchini.

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo