Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MHE. ABDALLAH: AIPONGEZA LATRA KWA UBORA NA UFANISI WA HUDUMA
Imewekwa: 30 Aug, 2024
MHE. ABDALLAH: AIPONGEZA LATRA KWA UBORA NA UFANISI WA  HUDUMA

 

Kamati ya Mawasiliano Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar imeipongeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa ubora na ufanisi wa kutoa huduma kwa wananchi na kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani Zanzibar (ZARTSA), katika utendaji kazi za Usafiri Ardhini.

Mhe.Yahya Abdallah Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, ameyasema hayo kwenye ziara ya siku moja ya Kamati hiyo ilioambatana na viongozi kutoka Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Ujenzi na Mawasiliano Zanzibar pamoja na Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani Zanzibar (ZARTSA), walipoitembelea Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) jijini Dodoma Agosti 29, 2024.

“Kikubwa ambacho tumeweza kukishuhudia sisi ni kuwaona wenzetu walivyopiga hatua kubwa ya ubora na ufanisi wa kutoa huduma zao kwa wananchi lakini kubwa zaidi na la kupendeza ambalo tumeweza kulishuhudia ni kuona jinsi taasisi ya LATRA na ZARTSA kwa upande wa Zanzibar na Serikali ya muungano wanavyoshirikiana katika utendaji wao wa kazi” amesema Mhe. Abdallah.

Aidha Mhe. Abdallah amebainisha kuwa na utofauti wa kisheria baina ya taasisi hizi mbili na kuongeza kuwa LATRA haina Mamlaka kisheria ya kuweza kutoa leseni za udereva kama ilivyo kwa upande wa ZARTSA.

“Ipo haja ya kuangalia hizi sheria na jinsi gani LATRA itaweza kupewa umiliki wa jukumu la kutoa leseni za udereva kisheria moja kwa moja, taasisi zetu zikae ziangalie njia bora ili kuhakikisha changamoto hii inatatuliwa na kuondosha usumbufu kwa wananchi wetu hilo ndo lengo la uwepo wa taasisi hizi” amesisitiza Mhe. Abdallah.

Kwa upande wake, Bw. Abdallah Mhagama, Kaimu Mkurugenzi Mkuu LATRA ameeleza lengo la ziara hiyo ni kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu udhibiti usafiri ardhini.

“Tuna fursa za kujifunza kutoka bara pamoja na visiwani, kuangalia mbinu tunazotumia huku na mbinu tunazotumia kule, mafanikio pamoja na changamoto, lakini kikubwa ambacho tumefarijika zaidi ni kwamba waheshimiwa hao wametumia usafiri wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es salaam mpaka Dodoma, na wamesifia sana huduma ile na kutupongeza kwa ubunifu tulioufanya kwenye maeneo mbalimbali ya kiudhibiti nchini” ameeleza Bw. Mhagama.

Aidha, Bw. Mhagama, ameihakikishia Kamati hiyo kuwa LATRA itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu, na kufanyia kazi ushauri uliotolewa kwa lengo la kuboresha huduma na shughuli zinazofanywa na Mamlaka na kuongeza kuwa  ipo haja ya kutengeneza utaratibu ambao msafiri kutoka Zanzibar anaweza akasafiri siku hiyo hiyo na kufika Dodoma.

 

Vilevile, Mhe. Fatma Ramadhani, Mjumbe wa kamati ya Mawasiliano Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, ameipongeza LATRA kwa kupiga hatua kwenye upande wa mifumo na kuipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukamilisha mradi wa reli ya kisasa (SGR).

“Kwanza niwapongeze LATRA kwa upande wa mifumo ya TEHAMA na pia nimpongeze kwa dhati Mama Samia kwa kukamilisha mradi kubwa wa Reli ya Kisasa (SGR) na mpaka leo tumesafiri kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma hatuamini, kwakweli nawapongeza sana ni hatua kubwa imefikiwa na LATRA kiukweli mtu aliyekuwepo nje ya nchi miaka sita akija Tanzania ya leo hawezi kuamini” ameeleza Mhe. Fatma

 

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo