Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MHE BABU: ZINGATIENI SHERIA, MIONGOZO NA TARATIBU ZA USAFIRISHAJI
Imewekwa: 05 May, 2023
MHE BABU: ZINGATIENI SHERIA, MIONGOZO NA TARATIBU ZA USAFIRISHAJI

Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu amewaasa madereva wa pikipiki za magurudumu mawili (bodaboda) na matatu (bajaji) kuzingatia Sheria, Miongozo na Taratibu za usafirishaji pindi wanapokuwa katika majukumu yao.

Mhe. Babu amesema hayo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kuanzisha chama cha ushirika cha watoa huduma za usafirishaji kwa njia ya bajaji na boda boda katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mjini na Moshi Vijijini tarehe 05 Mei, 2023 katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa, kilimanjaro.

“Kwa sasa tuna watoa huduma wengi wa usafirishaji kwa njia ya bajaji na boda boda katika Mkoa wetu. Wingi wetu unatakiwa kuendana sambamba na kuzingatia Sheria, Taratibu na kuhakikisha kuwa huduma tunazotoa zinakuwa za uhakika, kistaarabu, kuheshimiana na kushirikiana,“ameeleza Mhe. Babu.

Vilevile amewapongeza kwa kukubali na kushiriki katika kuanzisha ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) utakaowawezesha kupata fursa ya kujiwekea taratibu za utoaji huduma za usafirishaji, kupata mitaji kwa ajili kuboresha au kuongeza huduma pamoja na kupata elimu ya mara kwa mara ya biashara, usalama barabarani na masuala mengine na kukopeshana vitendea kazi.

Naye Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara kutoka LATRA Bw. Johansen Kahatano amesema SACCOS hiyo itawasaidia kuboresha maisha yao kijamii na kiuchumi kwa kuwa wataweza kukopesheka kupitia hisa zao na hatimaye kutoka kwenye kuajiriwa na kuwa na uwezo wa kujiajiri.

 “LATRA tupo pamoja na nyie katika hili na kupitia ushirika huu mtapata kamisheni ambayo itawasaidia kujikwamua kiuchumi na hivyo mtaweza kujitegemea. Kikubwa mjiepushe na migogoro isiyo na tija ili kufikia dira na malengo mliyojiwekea,“ amesisitiza Bw. Kahatano.

Vilevile amewataka madereva hao kuwa mabalozi katika kuhamasisha na kuratibu tuoaji wa elimu kwa watoa huduma wengine katika vituo mbalimbali vilivyopo Mkoani humo.

Kwa nyakati tofauti, madereva wa bajaji na bodaboda Mkoani Kilimanjaro wameishuru LATRA, Jeshi la Polisi pamoja na Kamati ya Uratibu wa Mchakato wa Uanzishwaji wa Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) kwa kuwezesha ushirika huo kwa kuwa utawasaidia katika kuanzisha miradi ya maendeleo itakayobadili maisha yao kiuchumi.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo