Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MHE. CHALAMILA: FUATENI SHERIA ZA NCHI, MFANYE BIASHARA KWA UHURU
Imewekwa: 08 Jan, 2024
MHE. CHALAMILA: FUATENI SHERIA ZA NCHI, MFANYE BIASHARA KWA UHURU

Mhe. Albert Chalamila, Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam amewataka wasafirishaji kufuata Sheria za nchi ikiwa ni pamoja na Sheria za Usalama Barabarani na Masharti ya Leseni zao ili kuboresha huduma za usafiri nchini na kuepusha migogoro na Mamlaka za Serikali zinazosimamia Sheria hizo.

Mhe. Chalamila ameyasema hayo kwenye kikao kati ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dar es salaam, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani pamoja Mmiliki wa kampuni ya Kilimanjaro Express, ili kujadili kufungiwa kwa kampuni hiyo Januari 8, 2023 Ofisi za LATRA Dar es Salaam.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Chalamila amemhimiza Mmiliki wa kampuni ya Kilimanjaro Express kufuata maagizo aliyopewa katika barua ya kufungiwa kutoa huduma ili kumuwezesha kufunguliwa na kuendelea kutoa huduma.

“Tumeweka Mfumo wa Tiketi Mtandao lakini bado kuna baadhi yenu mnakaidi, kwa kufanya hivi mazingira yenu ya kufanya kazi yatakuwa magumu mno, kuleta barua kwa Mamlaka na kuanza kufanya kazi wakati bado hamjaridhiwa na Mamlaka ni kiburi. Niwaombe msome kwa umakini kipengele cha nne cha barua yenu na mkitekeleze kama kilivyo ili muweze kuruhusiwa kutoa huduma,” amesema Mhe. Chalamila.

 Aidha, Mhe Chalamila amezihimiza Mamlaka zinazosimamia Sheria kufanya kazi kikamilifu na kuwaasa wasafirishaji wote kufuata Sheria za nchi badala ya kutegemea uhusiano walionayo na watu walio na nafasi mbalimbali katika jamii, ili kuweka jamii yenye ustawi bora na endelevu.

“Kwanza niwapongeze kwa hili na niwaombe tuendelee kuwa wakali kwani litakapoharibika jambo macho yote yatakuwa kwetu, namshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuliona suala la safari za saa 24, hii ni fursa nzuri hivyo muitumie kwa kutii Sheria, unaweza kufahamiana na mtu aliye madarakani leo akakusaidia lakini kesho hayupo madarakani na Sheria bado ipo, hivyo ni vyema kutii Sheria,” amesema Mhe. Chalamila.

Kwa upande wake CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA ameelezea hatua ambazo Mamlaka imezichukua kabla ya kuichukulia hatua kampuni hiyo ya Kilimanjaro Express.

“Disemba 22, 2023 tulifanya ukaguzi usiku na moja ya sehemu tuliyopita ni ofisi ya Kilimanjaro Express, tulikuta abiria wamezidishiwa nauli, tuliamuru kiasi kilichozidi kirudishwe na wakafanya hivyo, pia tuliwasiliana na  kituo cha Taifa cha Kutunza Data Kimtandao (NIDC) na wakatueleza kuwa mtoa huduma huyu alikwenda kwa ajili ya kufanya majaribio ya kutumia Mfumo wa Tiketi Mtandao na si kuanza kutumia, hivyo Januari 6, 2024 tukiwa kwenye ukaguzi tukapita katika ofisi yao na kukuta wamewazidishia tena nauli abiria na hawatoi Tiketi za Kielekroni, hivyo tukaamua kuchuka hatua kwa mujibu wa Sheria,” amesema CPA Suluo.

Naye SACP Ramadhani Ng’anzi, kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani amewaasa wasafirishaji wote kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa ili huduma inayotolewa iwe bora na yenye kugusa maslahi ya pande zote wasafirishaji, abiria na Serikali.

“Kilimanjaro Express kama wasafirishaji wengine anapaswa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa, Serikali inategemea sekta binafsi kwenye usafirishaji lakini haimaanishi wasafirishaji wapo juu ya Sheria, ndiyo maana hata leo asubuhi tumezuia abiria wapya kukatishwa tiketi, wanafunzi na wazazi waliokuwa na wekesho la safari ikafanyika busara ya kuwasafirisha kwa kibali maalumu, na huo ndio msimamo wetu,” amesema SACP ng’anzi.

Wakili Dickson Ngowi ni mwanasheria wa kampuni ya Kilimanjaro Express, na anakubali kutendeka kwa makosa na kuahidi kutojirudia huku maelekezo ya mwanzo ya Mamlaka yakiwa yamefanyiwa kazi.

“Aliyoyasema Mkurugenzi wa LATRA ni sahihi, tumekubali kuwa kuna makosa yametokea na ni makosa ya kibinadamu, hivyo kwa niaba ya Kilimanjaro Express napenda kuomba radhi kwa Serikali na wananchi ambao tunawahudumia na tunaahidi kuwa haitajirudia tena,” amesema Wakili Ngowi.

Januari 6, 2024, LATRA ilifanya ukaguzi wa kushtukiza katika Kituo Kikuu cha Mabasi Magufuli na ofisi ya Kilimanjaro Express ili kukagua hali ya usafiri na utekelezaji wa masharti ya leseni. Katika ukaguzi huo Mamlaka ilibaini kampuni ya Kilimanjaro Express kuwa na makosa kadhaa, ikiwemo kutoza nauli kubwa kuliko iliyoidhinishwa na Mamlaka na kutotoa tiketi za kielekroni likiwa ni kosa la kujirudia, hii ikasababisha kampuni hiyo kufungiwa kuanzia Januari 8, 2024 mpaka watakapotimiza vigezo walivyowekewa.

Vigezo ambavyo kampuni hiyo imepewa ni pamoja na kuanza kutumia mfumo wa Tiketi Mtandao ulioidhinishwa na Mamlaka, kuingiza nauli zisizozidi kiwango kilichoidhinishwa na Mamlaka na kuwasilisha maombi kwa Mamlaka yakionesha namna watakavyodhibiti makosa kama hayo kwa siku za usoni.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo