Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

DKT. ALLY POSSI: TRC, TAZARA BORESHENI MIUNDOMBINU YA RELI
Imewekwa: 14 Oct, 2023
DKT. ALLY POSSI: TRC, TAZARA BORESHENI MIUNDOMBINU YA RELI

Dkt. Ally Possi, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi ameagiza Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia (TAZARA) kurejesha upya alama za usalama wa reli kwa maeneo yote ambayo alama zimeondolewa au kuharibika. 

Ameyasema hayo tarehe 13 Oktoba, 2023 katika kilele cha Maadhimisho ya wiki ya Usalama wa Reli yaliyofanyika nchi za Jumuiya ya Mashirika ya Reli ya Kusini mwa Afrika (SARA) ambapo kwa upande wa Tanzania, maadhimisho haya yalifanyika kitaifa mkoani Tabora.

Dkt. Possi amezitaka taasisi zinazo simamia usafiri wa reli kuboresha miundombinu ya reli iliyoharibika ili tuhakikishe uwepo wa usalama na Usafiri bora kwa wananchi.

“Boresheni miundombinu hasa katika sehemu ambazo zimeharibiwa na wananchi na wamekuwa wakisababisha hasara kwa Serikali, Kwa wakandarasi na taasisi zetu sote tunapojenga miundombinu yetu tuhakikishe tunazingatia na kuboresha usalama wa wananchi” Amesema Dkt. Possi.

Aidha, amewasihi watanzania wote wawe walinzi wa miundombinu ya reli kwa maendeleo yetu wote, kwa kuwa wapo watu au kundi la watu wanaohujumu miundombinu ya reli na huo ni uhalifu, na kuwataka wananchi kutoa taarifa haraka kwa mamlaka za Serikali na Jeshi la Polisi

“Nitoe rai kwa wananchi na sisi sote kwa ujumla kutunza miundombinu, kwani tunapo iharibu ndipo tunapo hatarisha pia usalama wa usafiri wetu wa reli hivyo basi ukiona mtu au kundi la watu linahujumu miundombinu ya reli, huo ni uhalifu, na pia ni uhujumu uchumi, na kamwe Serikali hatuwezi kufumbia macho swala hili” Amesema Dkt. Possi .

Vilevile amesisitiza kuwa wananchi wanaoishi maeneo ya karibu na reli waendelee kukumbushana umuhimu wa kutunza na kulinda miundombinu na mazingira ya reli. 

“Naomba nitumie fursa hii kutoa wito kwa wananchi wanaoishi maeneo inakopita reli na watanzania wote kwa ujumla, waendelee kukumbushana umuhimu wa kutunza na kulinda miundombinu ya reli pamoja na mazingira yake kwa maendeleo ya nchi yetu, kwa kuunga mkono juhudi za dhati za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika uwekezaji mkubwa unaoendelea kwenye sekta ya reli ili kuboresha miundombinu ya reli zetu na kukuza uchumi wa Tanzania” Amesema Dkt. Possi.

Vilevile ameilekeza TRC kukamilisha kwa wakati ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa kipande kinachoanzia Dar es Salaam mpaka Morogoro na Morogoro mpaka Makutoporo kwa sababu ujenzi umechelewa sana kukamilika na wananchi wanahamu ya kupanda treni kutoka Dar es Salaam hadi Makutoporo.

“Nitoe maelekezo kwa TRC kuhakikisha kipande cha kwanza na cha pili kinakamilika kwa wakati, kwa sababu imechukua muda mrefu na wananchi wanahamu ya kupanda treni kutoka Dar es Salaam hadi Makutopora” Ameeleza Dkt. Possi.

Aidha Dkt. Possi ametoa taarifa kwa wananchi kuwa Wizara ya Uchukuzi inashirikiana na TAZARA katika hatua ya kuboresha miundombinu ya TAZARA kwa dhumuni la kukuza uchumi na kuboresha utoaji huduma kwa kuwa itasaidia usafirishaji wa mizigo hususan kutoka bandari ya Dar es Salaam mpaka nchi jirani.

“Nitoe taarifa kwa wananchi kuwa Wizara ya Uchukuzi kwa kushirikiana na TAZARA tupo katika hatua ya kuboresha miundombinu na wote tunafahamu sekta ndogo ya reli ni kichocheo cha uchumi lakini pia ni kichocheo kikubwa cha utoaji huduma kwani reli itasaidia usafirishaji wa mizigo hususan kutoka bandari yetu ya Dar es Salaam mpaka nchi jirani na ndani ya nchi yetu, wananchi watakuwa wanapata huduma ya usafiri wa reli kwa raha. Kwa bahati nzuri Serikali imepitisha bajeti ya kuendeleza miundombinu hii pamoja na kuhakikisha usalama wa wananchi unaendelea kutunzwa” Amesema Dkt. Possi.   

Kwa upande wake Prof. Ahmed Muhammed Ame, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Amesisitiza juu ya matumizi ya mifumo ili kuongeza ufanisi katika sekta ya usafirishaji kwa kuongeza usalama na kukuza uchumi katika Usafiri wa reli.

“Nipende kusisitiza juu ya mifumo katika kuongeza ufanisi, hii ni pamoja na Mfumo wa kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) na mfumo wa Tiketi Mtandao ili kuongeza usalama na kuhakikisha ufanisi wa kiuchumi katika reli zetu na yote haya yanawezekana iwapo tutaamua kubadilika” Amesema Prof. Ame.

“Napenda kuwakumbusha waendeshaji wa huduma za reli nchini, TRC na TAZARA kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za uendeshaji wa huduma za reli ili kuhakikisha usalama na kutoa huduma kwa ufanisi ikiwemo treni kufika vituoni kwa wakati” Ameongeza Prof. Ame.

Vilevile  amewataka vijana waliofuzu mafunzo yaliyoandaliwa na ofisi ya Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Tabora kutengeneza vikundi vya ushirika ili waweze kupeana elimu wenyewe kwa wenyewe na LATRA itawatumia kama waratibu wake kwa kutoa leseni kwa vijana wenye bodaboda mkoani Tabora.

Naye Mha. Hanya Mbawala Kaimu Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri wa Reli kutoka LATRA, Ameeleza kuwa LATRA inajukumu kubwa sana katika kudhibiti Usafiri wa reli kwa kutoa ithibati ya vitendea kazi, miundombinu na mabehewa ya treni ili kuhakikisha reli inafanya kazi kwa usalama kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zilizowekwa.

“Wananchi wengi wanaiona LATRA kwa upande wa Barabara tu lakini jukumu kubwa ni katika usafiri wa reli kwa kuhakikisha inafanya kazi kwa usalama kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa kwa kutoa ithibati ya vitendea kazi, miundombinu  na mabehewa, haya yote ni kuhakikisha Usafiri salama kwa wananchi pamoja na kukuza uchumi kwa ujumla” Amesema Mha. Mbawala.

“Hivi karibuni tutaanza majaribio ya Reli ya Kisasa (SGR) na tunatoa wito kwa wananchi wasiingie katika uzio wa SGR kwa sababu watapata madhara makubwa ambayo yanaweza kugharimu maisha yao” Ameongeza Mha. Mbawala.

Maadhimisho haya ya wiki ya Usalama wa Reli yenye kaulimbiu ya usalama unaanza na wewe, chukua tahadhari” yalifanikisha utoaji wa elimu kwa makundi mbalimbali ya wananchi wa Tabora na taasisi zinazosimamia usafiri wa reli zinatoa wito kwa wananchi na madereva wa vyombo vya moto wanatakiwa kuchukua tahadhari endelevu wanapotumia miundombinu ya reli.

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo