Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mhe. Daniel Baran Sillo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Agosti 26, 2024 wamekabidhi tuzo kwa wasafirishaji Bora na Salama kwa mabasi ya njia ndefu katika sherehe za ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani yanayofanyika kitaifa uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Tuzo hizo zimetolewa kufuatia shindano la kutafuta Watoa huduma Bora na Salama kwa huduma zilizotolewa Juni, 2023 hadi Julai 2024 kwa makundi ya Wasafirishaji Wakubwa, Wakati na Wadogo lililoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ikiwa ni sehemu ya kuchochea ushindani wenye ufanisi katika huduma za usafiri wa mabasi.
Akizungumza mbele ya Mhe. Dkt. Mpango, CPA Habibu J. Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA, amesema Kifungu cha 6(a) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura ya 413, kimeipa LATRA wajibu wa kuhamasisha ushindani wenye ufanisi miongoni mwa watoa huduma zinazodhibitiwa. Ameeleza kuwa, utoaji wa tuzo za Wasafirishaji Bora na Salama, ni sehemu ya utekelezaji wa wajibu huo.
Vilevile amewataja washindi kundi la Wasafirishaji Wakubwa (wenye mabasi zaidi ya 30) kuwa ni, Kampuni ya Shabiby Line mshindi wa kwanza, akifuatiwa na mshindi wa pili kampuni ya Happy Nation na mshindi wa tatu ni kampuni ya ABC Upper Class. Pia CPA Suluo amesema kuwa, kundi la pili (wenye mabasi 11 hadi 30) washindi ni kampuni ya Tilisho ambayo ni mshindi wa kwanza, ikifuatiwa na mshindi wa pili Satco Express na mshindi wa tatu ni Ngasere Co. Ltd.
Ameongeza kuwa, kwa kundi la Wasafirishaji Wadogo (wenye mabasi 3 hadi 10), mshindi kwa kwanza ni Sama Luxury Coach, wa pili ni kampuni ya Achimwene Business na wa tatu ni RATCO Express. Tuzo hizo zimetolewa ili kuchochea matumizi ya mifumo ya utoaji wa huduma bora na salama ya usafirishaji wa abiria kwa ufanisi na ubunifu hususan katika matumizi ya teknolojia.
Aidha, CPA Suluo alifafanua kuwa, mchujo ulifanyika kwa kuzingatia taarifa za mifumo LATRA ya utoaji huduma ambapo wasafirishaji wenye matukio mengi ya ajali, kuchezea Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Mabasi, kutoa huduma bila kuwa/kukata bima chini ya viwango stahiki, kusitishiwa leseni za usafirishaji kutokana na kutozingatia Sheria na Kanuni, malalamiko ya wateja kuhusu huduma zisizoridhisha, kutowapatia abiria tiketi za kielektroni, upotevu wa mizigo ya abiria, kuzidisha nauli na makosa mengine ya aina hiyo kwa idadi inachofikia 10% ya idadi ya mabasi waliyonayo waliondolewa katika kushindania tuzo hizo.
‘Kwa utaratibu huo idadi ya washindani ilipunguzwa hadi kubaki na washindani 15 kwa kila kundi (wakubwa, wa kati na wadogo). Washindani hao 15 kwa kila kundi waliwekwa katika dodoso la kidigitali lilitosambazwa kupitia tovuti ya LATRA na mitandao ya kijamii ili wadau na watumia huduma wawapigie kura, ambapo jumla ya wadau 2,237 walipiga kura kumchagua msafirishaji bora na salama.’ Alisema.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo, Bw. Florence Shirima, muwakilishi wa kampuni ya mabasi ya Tilisho Safaris amesema siri kubwa ya ushindi wao ni kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na kutoa huduma bora kwa wateja.
“Tunashukuru kwa ushindi huu tuliopata, kweli tumefarijika sana na tunaahidi kuendelea kuboresha huduma zetu ili mashindano yajayo tuweze kuibuka kidedea, Pia tunawashukuru wateja wetu kwa kutupigia kura kwa wingi na hatimaye kupata ushindi huu mnono, tunawaambia kuwa tuzo hii ni yao,” amesema Bw. Florence.
Kwa upande wake, Bi Stella Nestory, Meneja wa kampuni ya mabasi ya Sama Luxury Coach amewashukuru wadau waliowapigia kura na amesema kuwa tuzo waliyopata imewapa motisha ya kufanya kazi kwa ufanisi na kuongeza kasi ya utoaji wa huduma bora kwa wateja wao na wanaamini watafanya vizuri zaidi mashindano yajayo.
Bw. Priscus Joseph, Katibu Mkuu Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) ameipongeza LATRA kwa kutoa tuzo hizo kwa wasafirishaji wa mabasi ya masafa marefu nchini na amesema ni kiashiria tosha cha kuwatambua na kuwathamini wasafirishaji hao na itakuwa chachu kwa wamiliki wa kampuni za mabasi kuongeza juhudi ya kazi na ubora wa huduma.
“Tuzo hizi pia zitaongeza zaidi uhusiano na ushirikiano wetu na LATRA, ni mwanzo mzuri naipongeza sana LATRA na uongozi mzima kwa kufanikisha hili. Pia natoa wito kwa wasafirishaji kutoa huduma nzuri ili waweze kushinda na kupata tuzo,” ameeleza Bw. Priscus.
Kwa upande wake Bw. Ramadhani Msangi, balozi wa usalama barabarani amesema tuzo zilizotolewa zinaonesha jinsi Mamlaka inavyothamini wasafirishaji na lengo ni zuri la kuendelea kuchochea ushindani na kuwahamasisha kutoa huduma bora na salama kwa wateja wao.
Wakati huo huo, Mhe. Sillo amekabidhi vyeti maalum vya utambuzi kwa vyama vya wasafirishaji abiria na mizigo vilivyofanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na LATRA hivyo kuiwezesha mamlaka hiyo kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi. Vyama vilivyokabidhiwa vyeti vya utambuzi ni Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA), Chama cha Wamiliki wa Malori Wadogo na Wakati Tanzania (TAMSTOA), Chama cha Wasafirishaji Tanzania (TAT) na Chama cha Wasafirishaji Mizigo kwa Njia ya Barabara Tanzania (TRFA).
Pia Mhe. Sillo amekabidhi cheti cha utambuzi kwa Chama cha Ushirika na Mikopo cha Watoa Huduma za Bajaji za Abiria na Bodaboda Mkoani Kilimanjaro (KIBABOT SACCOS) kwa kutambua juhudi za cha hicho ambacho ni chama cha kwanza kutoa leseni za LATRA kwa pikipiki za magurudumu mawili na matatu kwa wanachama wao.