Mhe. David Kihenzile (Mb), Naibu Waziri wa Uchukuzi ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kazi nzuri inayotekeleza ikiwemo kubuni na kutumia mifumo mbalimbali ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo imerahisisha upatikanaji wa huduma za usafiri kwa abiria na watumiaji wengine ikiwemo mfumo wa Safari Tiketi unaowezesha ukataji wa tiketi za mabasi yote na tiketi za treni, Mfumo Tumizi wa LATRA (LATRA App) unaowezesha taarifa kwa abiria wa mabasi ya mikoani na nchi jirani na Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS).
Mhe. Kihenzile ametoa pongezi hizo Desemba 15, 2025 alipotembelea banda la LATRA katika maonesho ya Mkutano wa 18 wa Tathmini ya Utendaji wa Sekta ya Uchukuzi unaofanyika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) na kushuhudia shughuli za Udhibiti zinazotekelezwa na LATRA.
Kwa upande wake, CPA, Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA, amesema kuwa, LATRA imejipambanua kwenye matumizi ya mifumo mbalimbali ya TEHAMA na itaendelea kusimamia utekelezaji wa maono ya viongozi wa Nchi kwa kuongeza ufanisi katika usafirishaji wa abiria na mizigo katika sekta zinazodhibitiwa nchini.
Mkutano huo wa siku tatu unafanyika AICC kuanzia Desemba 15 hadi 17, 2025 ambapo kaulimbiu ni Mifumo Jumuishi ya Usafiri kama Nguzo ya Mageuzi ya Kiuchumi.

