Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MHE. KIHENZILE AIPA TANO LATRA KWA KUTUMIA MFUMO WA VTS
Imewekwa: 22 Nov, 2023
MHE. KIHENZILE AIPA TANO LATRA KWA KUTUMIA MFUMO WA VTS

Mhe. David Mwakiposa Kihenzile (Mb) Naibu Waziri wa Uchukuzi ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kutumia Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ajali za barabarani na athari zitokanazo na ajali. 

Mhe. Kihenzile ameyasema hayo Novemba 20, 2023, alipotembelea ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam na Kituo cha Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) kilichopo Mikocheni Jijini Dar es Salaam na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mamlaka ikiwemo utoaji wa leseni pamoja na usajili na uthibitishaji wa madereva wa vyombo vya moto kibiashara.

“Napenda kuipongeza LATRA kwa kazi nzuri na nimefurahishwa kuona jinsi nchi yetu ilivyopiga hatua kubwa katika teknolojia ya kudhibiti magari kupitia mfumo wa VTS, kwa kiwango kikubwa umepunguza ajali za barabarani ukilinganisha na kipindi cha nyuma ambapo VTS ilikuwa bado haijaanza kutumika nchini,” alisema Mhe. Kihenzile. 

Ameongeza kuwa, “Ufanisi wa mfumo huo ndio uliifanya Serikali iruhusu magari ya abiria kufanya kazi saa 24 kwa kuwa iliamini upo mfumo unaofanya kazi usiku na mchana hata kama askari wa usalama barabarani hawapo.”

Vilevile, amewataka madereva kuendelea kujitokeza kwa wingi kusajiliwa na kuthibitishwa na LATRA na kutii Sheria za Usalama Barabarani ikiwemo kuacha kuingilia mfumo wa VTS ili kuepusha ajali na vifo visivyokuwa vya lazima.

“Napenda kutoa wito kwa madereva kuendelea kutii Sheria za Usalama Barabarani na wawaonee huruma wananchi wanaopoteza maisha bila sababu za msingi kwa kuwa tunapoteza nguvu kazi ya Taifa, nawasihi madereva wajitokeze kusajiliwa na kuthibitishwa na LATRA ili kuwatambua madereva wanaokuwa safarini wakiendesha vyombo vya moto kibiashara na kupunguza changamoto zinazojitokeza barabarani,” alieleza Mhe. Kihenzile.

Kwa upande wake, Prof. Ahmed Mohamed Ame, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi LATRA, amemshukuru Mhe. Kihenzile kwa kuitembelea ofisi ya LATRA Mkoa wa Dar es Salaam na amemuahidi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kuwezesha mfumo wa VTS kutuma namba ya malipo (control number) moja kwa moja pale dereva anapokiuka Sheria kama ilivyokuwa hapo awali.

“Mfumo unaweza kufanya mambo mengi ikiwemo kutuma moja kwa moja namba ya malipo kwa kutoa adhabu moja kwa moja kwa madereva wanaokiuka Sheria za barabarani na kwa sasa tunaendelea kuzungumza na wenzetu Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani ifike mahala mfumo uweze kufanya hivyo kwasababu ulishawahi kufanya hivyo huko nyuma. Mfano katika ziara hii ya Mhe. Kihenzile niliangalia kwenye mfumo wa VTS na kuona dereva mmoja ametumia kifaa cha (I- Button) kuwasha magari matatu kwa pamoja na kuwapa madereva tofauti kuendesha lakini sisi mfumo ulitujulisha,” alisema Prof. Ame.

Naye Bw. Johansen Kahatano, Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara kutoka LATRA alieleza kuwa, usajili wa madereva unaenda vizuri, hadi sasa madereva 2,757 wawameshafanya mtihani wa kuthibitishwa na LATRA na madereva 1,817 wamefaulu na waliofeli wanayo fursa ya kurudia mtihani huo.

“Kutokana na matukio ya ajali yanayojitokeza tumefanya tathmini na tumepata faraja kuona kwamba tangu mwezi Septemba hadi sasa wale madereva wachache tuliowathibitisha wanafanya vizuri barabarani na kubaini wachache ndio wanaokiuka Sheria  lakini bado tunaendelea kuwafuatilia kila siku hususan kwenye safari za usiku, itambulike kuwa katika kuchukua hatua za Kisheria haijalishi dereva awe amethibitishwa au hajathibitishwa iwapo atabainika kuvunja Sheria tutampatia adhabu,” alieleza Bw. Kahatano.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo