Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MHE. KIHENZILE AKOSHWA NA UBUNIFU WA MIFUMO YA LATRA
Imewekwa: 20 Jun, 2025
MHE. KIHENZILE AKOSHWA NA UBUNIFU WA MIFUMO YA LATRA

Mhe. David Mwakiposa Kihenzile (Mb), Naibu Waziri - Uchukuzi ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa utendaji kazi na ubunifu wa mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo imerahisisha utoaji wa huduma kwa wadau.

Mhe. Kihenzile ametoa pongezi hizo Juni 19, 2025 alipotembelea banda la LATRA kwenye Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.

“Nawapongeza sana LATRA kwa kuendelea kuwa wabunifu wa mifumo mbalimbali ambayo mnaitumia kurahisisha huduma za usafirishaji nchini mfumo wa kwanza ni  mfumo wa kufuatilia mwenendo wa magari (VTS) ambao wananchi wameupokea vizuri sana kwa kuweza kuona chombo kipo wapi na kinatembea kwa mwendokasi gani na tunategemea kufanya tathmini baada ya mwaka mmoja kujua kama ajali za barabarani zimepungua.” amesema Mhe. Kihenzile

Naye, Bw. Ezekiel Emmanuel, Afisa Mfawidhi LATRA Dodoma, alimueleza Mhe. Kihenzile kuwa, Mamlaka inatekeleza kwa vitendo maelekezo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kubuni na kutumia Mifumo ya TEHAMA inayoongeza tija ya utendaji kazi na usimamizi wa huduma.

Vilevile Bw. Emmanuel amesema kuwa, ili kuongeza tija ya udhibiti wa sekta ya usafiri ardhini pamoja na kuongeza wigo wa kufuatilia mwenendo wa mabasi, LATRA imewezesha upatikanaji wa taarifa za mabasi kupitia Mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS) unaopatikana kwa anwani pis.latra.go.tz/ uliounganishwa na mfumo mama wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) ambao umeleta manufaa makubwa kwakuwa umechangia sana kubadilisha tabia za madereva wanapokuwa barabarani na chombo cha moto.

 “LATRA inagusa abiria na watoa huduma wa kawaida kabisa na tumeweza kuboresha huduma kwa kuanzisha mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS) unaomuwezesha abiria kujua mahali basi lilipo na mwendo kasi wa basi, mfumo huo umetokana na mfumo mama wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) unaoweza kudhibiti mwendokasi wa mabasi ya masafa marefu, amefafanua Bw. Emmanuel.

Ameongeza kuwa LATRA kwa sasa imerahisisha huduma za utoaji wa leseni ambapo mtoa huduma anaweza akaomba leseni bila kuwa na haja ya kufika ofisini kwa kuingia tu kwenye mfumo wa Usimamizi wa Reli na Barabara (RRIMS) kwa anuani https://rrims.latra.go.tz  na kufanya maombi ya leseni na kupata  namba ya kumbukumbu ya Malipo popote pale alipo na akisha lipia anaweza kuchapa leseni yake.

 Aidha, Bw. Emmanuel ameitaja mifumo mingine inayotumiwa na LATRA ni Mfumo Tumizi wa LATRA (LATRA App), Safari tiketi, mfumo wa Uthibitishaji wa Madereva (DTS) pamoja Mfumo wa Taarifa kwa abiria (PIS).

LATRA inashiriki kwenye maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma  jijini Dodoma kuanzia Juni 16 hadi 23, 2025 ambapo wadau wa sekta ya usafiri ardhini wanapatiwa elimu kuhusu mifumo mbalimbali inayotumiwa na Mamlaka katika kutekeleza majukumu yake kwa ubora na ufanisi.

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo