
Mhe. Abubakar Kunenge, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, amefunga rasmi semina ya kuwajengea uwezo Wanahabari Mabalozi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), huku akiwapongeza wanahabari hao kwa kuwa kinara kutenga muda wao kuhudhuria semina hiyo iliyoandaliwa na LATRA.
Pongezi hizo amezitoa Mei 7, 2025 ukumbi wa TARI- Kibaha Mkoa wa Pwani ambapo Wanahabari Mabalozi 40 kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini walijengewa uwezo kuhusu uandishi wa habari za LATRA pamoja na kufahamu kazi na majukumu ya Mamlaka.
“Namshukuru CPA Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA kwa kunialika rasmi kufunga semina hii ambayo mmeiendesha hapa katika Mkoa wangu, jambo hili ni zuri naamini waandishi hawa wakitoka hapa watakuwa mahiri zaidi na watatumia kalamu zao vizuri katika kuelimisha jamii kuhusu masuala yanayohusu sekta ya usafiri ardhini nchini pamoja na jitihada za kuboresha sekta ya Usafiri Ardhini zinazotekelezwa na Serikali yetu ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Mhe. Kunenge.
Mhe. Kunenge ameongeza kuwa, Mhe. Dkt. Raisi Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa ni kiongozi wa kuigwa kwa kuwa amekuwa kinara katika utendaji wa majukumu ya nchi ambapo amefanya jitihada kubwa kuboresha barabara mkoa wa Pwani zinazochochea ukuaji wa uchumi kwa haraka kwa wananchi.
Vilevile, amempongeza CPA Suluo na Menejimenti yake kwa jitihada wanazozifanya katika udhibiti wa sekta ya usafiri ardhini nchini na pia kwa kuwa na uhusiano mzuri na wadau wakiwemo wanahabari ambao wamekuwa wakisaidia kufikisha taarifa za LATRA na Serikali kwa wananchi kwa wakati mwafaka.
Naye CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA alimueleza Mhe. Kunenge kuwa, semina hiyo imeendeshwa kwa siku mbili yaani Mei 6 na 7, 2025 na Mamlaka itaendelea kufanya kazi kwa karibu na ushirikiano na wanahabari nchini kwa kuwa wanafanya kazi kubwa ya kuhabarisha na kuelimisha umma kuhusu masuala mbalimbali yanayojenga Taifa na yanayoakisi maono na falsafa za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.