Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MHE. LUDIGIJA AFUNGUA MKUTANO WA WADAU WA TEKSIMITA
Imewekwa: 14 Dec, 2022
MHE. LUDIGIJA AFUNGUA MKUTANO WA WADAU WA TEKSIMITA

Na Mambwana Jumbe

Mkuu wa Wilaya Ilala Mhe. Ng'wilabuzu Ndatwa Ludigija amesema Serikali ya awamu ya Sita, inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassani  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya juhudi za kipekee kuhakikisha inakuza sekta binafsi kwa kuhakikisha sekta hiyo inakuwa chachu ya kusukuma uchumi na chanzo cha mapato ya serikali kupitia kodi na kuongeza ajira kwa vijana hasa kwenye huduma za usafiri ardhini ikihusisha magari ya kukodi na huduma za usafiri wa mijini kwa kutumia mabasi na pikipiki za miguu miwili na mitatu.

Mhe Ludigija amesema hayo Desemba 14, 2022 katika Ukumbi wa Mkutano Karimjee jijini Dar es Salaam alipofungua mkutano wa wadau wa kupokea maoni ya kuhusu utaratibu wa matumizi ya mita za teksi (taximeter) kwenye usafiri wa teksi za kawaida ambazo hutumika kwa kukodishwa kwa safari binafsi hapa nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam Mhe. Amos Makala, Mhe. Ludigija amesema kuimarika kwa miundombinu ya barabara katika maeneo mengi hapa nchini imesaidia kuimarika kwa usalama na ubora wa huduma za  usafiri wa barabara na hivyo kuongeza kasi ya ukuaji uchumi.

Akizungumzia teksimita, Mhe. Ludigija alisema kuwa matumizi ya teksimita yatasaidia kukokotoa kiwango cha nauli atakachotakiwa kulipa mteja baaada ya kufika mwisho wa safari na hivyo aliwasihi wadau wote waliohudhuria kikao hicho kutumia fursa ya kutoa maoni ili kuwezesha upatikanaji wa mawazo chanya yatakayosaidia kupata utaratibu mzuri wa uendeshaji wa teksimita ili kila mmoja anufaike nazo,” alieleza

“Niwapongeze sana LATRA katika hili kwasababu wamekuwa wakishirikisha wadau kabla ya kufanya uamuzi kwenye masuala mbalimbali na hivyo nizisihi taasisi nyingine kuiga jambo hili jema linalofanywa na LATRA,” alisisitiza

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu LATRA, Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara LATRA Bw. Johansen Kahatano alisema “Jukumu hili la ushirikishaji umma ni zao la utawala bora ambapo inasisitizwa kushirikisha wadau kwenye utekelezaji wa majukumu ya kiudhibiti ambayo misingi yake imejengwa kwenye Sheria ya LATRA ya mwaka 2019 na kanuni zake.”

Vilevile Bw. Kahatano aliongeza kuwa kwa kutambua si kila mdau anaweza kufika katika mkutano huo, Mamlaka imeweka utaratibu wezeshi wa kuendelea kupokea maoni kwa njia ya maandishi hadi tarehe 31 mwezi Desemba mwaka huu ambapo mdau anaweza kuwasilishwa kwa kuyafikisha katika ofisi za Mamlaka zilizopo mikoa yote au kwa barua pepe ya dg@latra.go.tz.

Aidha alifafanua kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya LATRA na. 3 ya mwaka 2019 na kanuni ya 15 (d) ya LATRA ya Usafiri wa Kukodi ya mwaka 2020, Kanuni ya 15(d) inaelekeza kuwa vyombo vyote vinavyopewa leseni ya usafiri wa kukodi vinatakiwa kuwa na mita ya nauli au mfumo unaweza kukukotoa nauli.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo