Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MHE. MAJALIWA : LATRA NA TAMISEMI WAPATIENI ELIMU MADEREVA WA PIKIPIKI ZA MAGURUDUMU MAWILI
Imewekwa: 15 Mar, 2023
MHE. MAJALIWA : LATRA NA TAMISEMI WAPATIENI ELIMU MADEREVA WA PIKIPIKI ZA MAGURUDUMU MAWILI

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb)  ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupitia Mamlaka ya Serikali za mitaa kuwaratibu na kuwapa elimu madereva wa pikipiki za magurudumu mawili (Bodaboda).

Mhe. Majaliwa ameyasema hayo wakati akifungua rasmi maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani mwaka 2023 iliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, ambayo kitaifa inaadhimishwa Jijini Mwanza kuanzia Jumanne Machi 14, 2023 hadi Jumamosi Machi 18, 2023.

“Niwatake LATRA, mshirikiane na Ofisi ya Rais TAMISEMI kupitia  Mamlaka ya Serikali za Mitaa ili kuwafikia wasafirishaji wadogo wadogo maarufu kama bodaboda, kaeni nao pamoja wapatiwe elimu juu ya namna bora ya kuendesha vyombo vyao kwa usalama, lakini pia waratibiwe ili wajue namna bora ya kuendesha biashara yao” amesema Mhe. Majaliwa.

Aidha Mhe. Majaliwa amewataka Wananchi wa Mwanza na Tanzania kwa ujumla kuwa mstari wa mbele katika kukemea vitendo ambavyo vinaweza kusababisha ajali na kupelekea athari kubwa kwa Watanzania.

“Nimetazama igizo moja mtandaoni, abiria amemnyang’anya siti dereva kwa sababu dereva alikuwa anaongea na simu huku anaendesha, mara anashuka bila sababu ya msingi, akasema gari halitoki mpaka aje dereva mwingine, na nyie muwe hivyo, mkiona uendeshaji hatarishi msikae kimya, toeni  taarifa kwa mamlaka husika, hapo kila mtu atakuwa ametimiza wajibu wake na Tanzania bila ajali itawezekana.” Ameongeza Mhe. Majaliwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Jumanne Sagini (Mb) amewataka wamiliki wa vyombo vya moto kufuata maelekezo yaliyotolewa na Waziri wa mambo ya Ndani Mhe. Mha. Hamadi Masauni na kufunga vidhibiti Mwendo katika Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS).

“Kuhusu swala la kuchagua kimoja kati ya kidhibiti mwendo au VTS inayobeba dhana zote mbili, Waziri mwenye dhamana Mhe. Masauni ameshatoa maelekezo kuwa kwa kuwa vifaa vya VTS vinaweza kufungwa vidhibiti mwendo basi  wamiliki wa magari ya kusafirisha abiria wafunge vidhibiti mwendo kwenye mfumo huo” amesema Mhe. Sagini.

Akiongelea jitihada zilizofanywa na Baraza la Taifa la Usalama Barabarani katika kudhibiti ajali kutoka kwa madereva wa serikalini, Mhe. Sagini amesema Baraza kwa kushirikiana na LATRA, Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzani (TIRA) waliendesha mafunzo ya usalama barabarani kwa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuhakikisha madereva wao wanachukua tahadhari.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Hali ya Ajali kwa mwaka 2022, makosa ya kibinadamu bado yanachangia kwa kiasi kikubwa ajali zinazotokea nchini, hivyo basi ni vyema kila mmoja wetu akatimiza wajibu wake kikamilifu ili kuhakikisha tunapunguza hatari ya ajali tuwapo safarini.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo