
Mhe. Edward Mpogolo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala amewapongeza maafisa usafirishaji wa pikipiki za magurudumu mawili (Bodaboda) na pikipiki za magurudumu matatu (Bajaji) kwa kuanzisha Chama cha Ushirika cha Maafisa Usafirishaji wa Pikipiki Mkoa wa Dar es Salaam (MAUPIDA) kwa kuwa ushirika huo utawawezesha kujikwamua kijamii na kiuchumi ikiwemo kutoka kwenye kuajiriwa mpaka kujiajiri kwa kununua na kumiliki bajaji na bodaboda zao wenyewe
Mhe. Mpogolo amebainisha hayo wakati akikabidhi cheti cha ushirika kwa chama hicho katika hafla iliyofanyika Aprili 04, 2025 katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Ilala.
“Nawapongeza sana kwa kuanzisha ushirika wenu wa MAUPIDA na hakika ushirika huu utawawezesha kupata mikopo kwenye taaasisi za fedha na pia mtapata gawiwo la asilimia 20 kutoka LATRA,” amesema Mhe. Mpogolo.
Vilevile Mhe. Mpogolo ameihimiza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuwapatia uwakala MAUPIDA ili kukusanya mapato kwa niaba ya Mamlaka kwa kuwa zipo pikipiki zaidi ya 150,000 katika halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ndani na pembezoni mwa mji.
Naye Bw. Pateli Ngereza, Afisa Mfawidhi LATRA Mkoa wa Dar es Salaam, amesema kuwa uanzishwaji wa vyama vya ushirika kwa maafisa usafirishaji umekuwa ni tamanio la Mamlaka na ushirika huo utawezesha watoa huduma wote wa bodaboda na bajaji kupata leseni za LATRA popote walipo kupitia SACOSS yao.
“Hii imekuwa ni kiu yetu ya muda mrefu kuhakikisha kwamba tunawaweka kwa pamoja katika umoja ambao utakuwa na manufaa kwa wanachama, jamii na Serikali kwa jumla na tunaamini kuwa, baada ya kuanzisha SACOSS hii Mamlaka itaingia makubaliano kwa mujibu wa Kanuni za usafirishaji wa kukodi na vyama hivi ambavyo vimeanzishwa kisheria kwa ajili ya kutoa huduma kwa niaba ya Mamlaka. Na hii imekuwa msaada kwetu kuhakikisha kwamba chama hiki kinajisimamia na wanasimamiana wenyewe na watoa huduma wote wa bodaboda na bajaji wanapata leseni zetu popote pale walipo kwa SACOSS hii,” amefafanua Bw. Ngereza.
Kwa upande wake, Bw. Saidi Kagoma, Mwenyekiti wa ushirika huo ameishukuru Serikali kupitia LATRA kwa jitihada za kuinua hali za maisha ya maafisa wasafirishaji kwa kuwahamasisha kujiunga na kuanzisha vyamaa vya ushirika.
“Gharama ya leseni kwa bajaji ni TZS. 22,000/= na bodaboda TZS. 17,000/= na tumeelezwa kuwa tutapata gawio la asilimia 20 na pia tutaweza kukopesheka, hii ni faraja kwetu kwa kuwa tutaweza kuanzisha miradi mbalimbali itakayotuinua kiuchumi na kijamii na pia tunaamini na sisi tutamiliki magari kupitia ushirika wetu,” amesema Bw. Kagoma.
Kwa nyakati tofauti, wanachama wa MAUPIDA wameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuwatambua, kuwajali, kuwalea na kuwathamini, na pia wamefurahi kwa kuwa ushirika wao umepata baraka za Serikali kupitia LATRA na wanaamini hali zao za maisha zinaenda kubadilika kupitia ushirika huo.