Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MHE. MPOGOLO AWATUNUKU VYETI MADEREVA 1,518 WALIOTHIBITISHWA NA LATRA
Imewekwa: 04 Jun, 2024
MHE. MPOGOLO AWATUNUKU VYETI MADEREVA 1,518  WALIOTHIBITISHWA NA LATRA

Mhe. Edward Jonas Mpogolo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala amewatunuku vyeti madereva 1518 waliofanya mtihani na kuthibitishwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na hivyo kufikisha jumla ya madereva 2517 ikiwa ni pamoja na madereva 999 waliothibitishwa hadi Julai 1, 2023.

Mhe. Mpogolo amewatunuku madereva hao katika hafla ya pili ya utoaji vyeti kwa madereva waliothibitishwa na LATRA iliyofanyika Juni 04, 2024 katika ukumbi wa mikutano Arnaoutoglou uliopo Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Mpogolo amewaambia madereva kuwa vyeti walivyotunukiwa vitatambulika kitaifa na kimataifa hasa kwa Nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), hivyo ni manufaa makubwa kwa kuwa wanaenda kutanua wigo wa ajira ndani na nje ya nchi hatimaye watajiinua kiuchumi na kijamii.

Vilevile Mhe. Mpogolo amewapongeza madereva hao na amewaeleza kuwa, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawathamini na imedhamiria kuongeza hadhi ya madereva na ndio maana kupitia LATRA jambo hilo linafanyika, “Uthibitishaji huu wa madereva utawaheshimisha zaidi na maslahi yenu yataboreshwa na zaidi ya yote, taaluma hii ya udereva itarasimishwa na kukomesha tabia ya baadhi ya wasafirishaji kuwapa kazi ya udereva watu wasiostahili kufanya kazi hiyo.”

Kwa upande CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA amewasihi madereva wa vyombo vya moto kibiashara kujitokeza kusajiliwa na kuthibitishwa ili kuongeza thamani katika fani yao ya udereva ukizingatia kuwa suala hilo ni takwa la kisheria na amewasihi kujiendeleza zaidi ili Mamlaka ipate hoja za kurasimisha ajira zao.

Aidha ameeleza kuwa Mamlaka haitatoa leseni kwa basi ambalo halina dereva aliyethibitishwa na LATRA kufikia Julai Mosi, 2024 kwani Mamlaka ilitoa muda wa kutosha kutekeleza Sheria hii, “nawasihi wananchi wasikubali kuendeshwa na madereva wasioweza kufuatiliwa mwenendo wao, kwani wanaposababisha ajali hukimbia na niwasihi wasafirishaji kuwa milango ya kusikiliza wenye changamoto ipo wazi ili msikwame kuendelea kufanya biashara ya usafirishaji.”

Vilevile amesema kuwa, madereva waliothibitishwa watapatiwa kitufe cha utambuzi (i-button) chenye taarifa za kila dereva husika, na kitufe hicho ni mali ya dereva, sio mwajiri, na kinapaswa kutumika kila wanapoanza safari na kumaliza safari.

CPA Suluo ameongeza kuwa LATRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani imeandaa video za kuwakumbusha madereva kuhusu masuala ya msingi ya kuzingatia wakiwa barabarani ikiwemo suala la alama na michoro na video hizo zinapatikana LATRA Online TV kwenye mtandao wa YouTube na amewasihi madereva kujielimisha zaidi hata kama wameshapata cheti cha kuthibitishwa.

Akizungumza kwa niaba ya Dkt. Zainab Rashid, Mwenyekiti wa Kamati ya Uthibitishaji Madereva LATRA, Bw. Mohamed Mpinga Naibu Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Polisi  na Makamu Mwenyekiti wa Uthibitishaji wa Madereva, amewapongeza madereva waliojitokeza kufanya mtihani na kufaulu na anaamini wataenda kutekeleza kwa vitendo barabarani kwa lengo la kupunguza athari za ajali barabarani.

Katika kipindi cha kuanzia tarehe 01 Juni, 2023 hadi 31 Machi, 2024 Mamlaka ilisajili jumla ya madereva 8,729 kwenye kanzidata ya LATRA, ambapo kati yao, madereva 3,254 (sawa na asilimia 37.3) walijitokeza kufanya mitihani na madereva 1,518 wamefaulu na kuthibitishwa na LATRA.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo