Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MHE. MWAKIBETE AIPONGEZA LATRA
Imewekwa: 13 Oct, 2022
MHE. MWAKIBETE AIPONGEZA LATRA

Na. Mambwana Jumbe

Naibu Waziri Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Atupele Fredy Mwakibete (MB) ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kuendelea kudhibiti sekta ya usafiri wa reli na kuhakikisha kuna usalama kwenye sekta hiyo.

Mhe. Mwakibete amesema hayo Oktoba 13, 2022 alipokuwa akifunga maadhimisho ya Wiki ya Usalama wa Reli mwaka 2022 kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (MB).

Aidha, Mhe. Mwakibete amesema kuwa LATRA imekuwa ikifanya ukaguzi wa mara kwa mara ya miundombinu ya njia za reli na wanasimamia utekelezaji wa Sheria na kanuni zake kwa lengo la kuboresha kulinda miundombinu ya njia za reli nchini.

Mhe. Mwakibete amewataka wananchi wote wanaoishi maeneo yanayopita treni, kuchukua tahadhari ili kulinda maisha na mali zao “dhamira ya kaulimbiu ya maadhimisho haya inatutaka tuongeze umakini tuwapo katika maeneo ya njia za reli, hivyo niwaombe wananchi tuwe makini kuhakikisha kuwa shughuli za kijamii na kiuchumi hazifanyiki karibu ya miundombinu ya reli.”

Akizungumzia majukumu ya LATRA katika uendeshaji wa reli. Mkurugenzi Mkuu LATRA CPA Habibu Suluo amesema kuwa LATRA ni msimamizi mkuu wa usalama usafiri wa reli kwa kuhakikisha sharia na taratibu za uendeshaji wa reli unazingatiwa, pia inatoa ithibati kwa miundombinu mipya iliyojengwa ambapo kwa sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa reli ya kisasa SGR, LATRA itafanya uthibitishaji wa mradi mzima ili uweze kutumika kwa usalama.

Vilevile amesema, majaribio ya uendeshaji wa reli ya kisasa ya SGR unatarajiwa kuanza hivi karibuni, hivyo amewakumbusha wananchi kuchukua tahadhali kwa kutokufanya shughuli katika maeneo hayo, “treni za SGR zina mwendo kasi sana yaani km160 kwa saa, hivyo ni vema wananchi kuwa mbali na reli ili kuepusha madhara.”   

Vilevile CPA Suluo amewahimiza wananchi kuilinda miundombinu ya reli ili isihujumiwe na watu wachache wenye nia mbaya ya kuharibu uchumi ikizingatiwa kuwa, Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya reli na hivyo ni vema tukailinda kwa ajili ya kulinda uchumi wa nchi.

Wiki ya usalama Usafiri wa Reli ilianzishwa na wanachama wa SADC ili kutoa fursa kwa wananchi kufahamishwa matumizi sahihi ya reli katika usafirishaji wa abiria na mizigo. Wiki hii inaadhimishwa katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR. Hivyo kuwezesha usafirishaji kwa njia ya reli kuwa wa haraka na usalama zaidi. Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni Jihadhali, treni zina mwendo kasi na haziwezi kusimama ghafla.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo