Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

LATRA Logo

MHE. MWAKIBETE: WAKUU WA TAASISI MUWARUHUSU WATUMISHI KUSHIRIKI MICHEZO
Imewekwa: 21 Jan, 2023
MHE. MWAKIBETE: WAKUU WA TAASISI MUWARUHUSU WATUMISHI KUSHIRIKI MICHEZO

Na Mambwana Jumbe

Naibu Waziri Waziri Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) Mhe. Atupele Mwakibete amewataka Wakuu wa Taasisi walio chini ya Wizara yake kuwaruhusu watumishi wanamichezo kushiriki kwenye mabonanza mbalimbali ili kuimarisha afya zao.

Mhe. Mwakibete amesema hayo leo Januari 21, 2023 alipokuwa akifungua bonanza la Sekta ya Uchukuzi lililodhaminiwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na kufanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa, Mhe. Mwakibete amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo kwa watumishi kufanya mazoezi ili kuboresha afya zao na hivyo amewapongeza watumishi wa Sekta ya Uchukuzi kwa kuandaa na kushiriki bonanza hilo ambalo linaonesha dhahiri namna wanavyotekeleza agizo la Mhe. Rais Dkt. Samia Suhuu Hassan.

“Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa wananchi wafanye mazoezi kwa mustakabali mzuri wa afya zao na kwa hili mlilolifanya hapa leo kiukweli mmeonesha kwa vitendo kuwa mnatekeleza maono ya Rais wetu kwa vitendo”, amesisitiza Mhe. Mwakibete.

Vilevile Mhe. Mwakibete amewataka Wakuu wa Taasisi kuhakikisha wanatenga bajeti ya kutosha ili kuwawezesha watumishi wanamichezo kushiriki kikamilifu kwenye michezo na amesisitiza Wizara itahakikisha inasimamia utekelezaji wa jambo hilo.

“Serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa kwenye matibabu ya wananchi wake kwa sababu ya kutofanya mazoezi hivyo ninaendelea kuwasihi kufanya mazoezi kila mara ili kuepukana na magonjwa yanayosababishwa na tabiabwete,” ameeleza Mhe. Mwakibete.

Wakati huohuo Mhe. Mwakibete amezindua Jarida la Klabu ya Sekta ya Uchukuzi na amewapongeza viongozi wa Klabu hiyo kwa kubuni na kuandaa jarida hilo litakalotoa taarifa mbalimbali za michezo ya Sekta ya Uchukuzi.

Naye Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) CPA Habibu Suluo amemshukuru Mhe. Mwakibete kwa kujumuika pamoja kwenye bonanza hilo na amesema michezo ni afya, inaleta umoja na inaongeza ufanisi katika maeneo ya kazi.

“Ushiriki wako hapa leo umetupa nguvu kubwa ya kuendeleza michezo hii na tunaahidi kuendeleza ushirikiano huu uliopo miongoni mwetu kupitia michezo,” ameeleza CPA Suluo .

Naye Katibu wa Klabu ya Uchukuzi Bw. Mbura Tenga amesema hilo ni bonanza la tano kuandaliwa na Sekta ya Uchukuzi na ameishukuru LATRA kwa kudhamini kwa asilimia 100.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo