Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MHE. PROF. MBARAWA: SERIKALI KUFUNGUA NCHI NA KUBORESHA MIUNDOMBINU KATIKA SEKTA YA UCHUKUZI
Imewekwa: 15 Aug, 2024
MHE. PROF. MBARAWA: SERIKALI KUFUNGUA NCHI NA KUBORESHA MIUNDOMBINU KATIKA SEKTA YA UCHUKUZI

Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame M. Mbarawa(Mb) amesema Serikali inaendelea kujenga, kuboresha miundombinu ya uchukuzi na kufanya mabadiliko ya kimkakati katika sekta ya uchukuzi ili kufungua nchi na Mataifa mengine.

Mhe. Prof. Mbarawa ameyasema hayo, tarehe 14 Agosti, 2024 katika Ukumbi wa Mikutano wa Johari Rotana, jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Uchukuzi ulioandaliwa na Chama cha Wasafirishaji Mizigo cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (FEAFFA).

Mhe. Prof. Mbarawa ametumia fursa hiyo kuwaomba wadau wa sekta binafsi kuungana ili kuchangamkia fursa lukuki katika sekta ya Uchukuzi.

“Serikali imefanya marekebisho ya sheria namba 10 ya mwaka 2017 ili kuruhusu ushiriki wa sekta binafsi katika kutoa huduma kwa njia ya reli, hivyo pamoja na Shirikia la Reli Tanzania (TRC) kutoa huduma za reli, sekta binafsi inakaribishwa  kutoa huduma hiyo ili kuhakikisha wateja wananufaika na miundombinu hiyo, mwekezaji tunamkaribisha aje na  vichwa vyake pamoja na mabehewa yake  kutumia reli ya kisasa (SGR) na tunaamini TRC pekee hatoweza kutoa huduma peke yake, hivyo tunaamini kwa kushirkiana  na mashirika binafsi tunaweza tukaona mabadiliko makubwa katika sekta ya usafiri na usafirishaji” ameeleza Mhe. Prof. Mbarawa.

Aidha amesema mkutano huo  umekusudia  kujenga ushirikiano wa pamoja katika sekta ya uchukuzi, kuweka fursa ya kuongeza ufahamu, kutathmini maendeleo ya kimataifa na maendeleo ambayo Afrika na hasa kanda ya Afrika Mashariki imefanya, kuangazia vikwazo na kupendekeza namna ya kusonga mbele kwenye sekta ambayo ni kitovu cha Uchumi.

“Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huu ni fursa kubwa kwa uchumi wa nchi kwani Tanzania ni lango kuu kwa kuhudumia mizigo ya nchi saba za wanachama za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika na hii inatokana na Tanzania kuwa na njia kuu tisa za usafiri wa barabarani kwenye shoroba za ukanda wa TANZAM, wa kaskazini mashariki, kusini pwani kati maziwa makuu, wa kusini, wa magharibi, wa Kati na Ukanda mkuu wa Kaskazini” ameeleza Mhe. Prof. Mbarawa

Vile vile kwa upande wake Rais wa Chama cha Wakala wa Forodha (TAFA),Bw.  Edward Urio amesema kuwa mikutano kama hii ni fursa kwa serikali kuweza kuelezea mipango yake, mikakati yake na pia kupitia wizara ya uchukuzi imewahakikishia wadau wa sekta binafsi kuwa kuna baadhi ya sera zitafanyiwa kazi na zitaleta manufaa kwa nchi.

Aidha Mhe. Prof. Mbarawa ameeleza kuwa kwa upande wa reli ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) serikali imeanza kufanya ukarabati wa njia ya reli ya zamani ya (meter gauge) kwa kuboresha njia mpya kwa kubadilisha reli nzito na kuimarisha madaraja kati.

“Lengo kuu la serikali ni kuhakikisha reli hiyo ya zamani (meter gauge) inafanya kazi ipasavyo na inachangia kwa kiasi kikubwa sekta ya usafirishaji na logistiki, serikali ya awamu ya sita pia imefanya ujenzi wa reli mpya ya kisasa (SGR) yenye urefu wa kilometer 1219 kwa awamu ya kwanza na awamu ya pili yaani kutoka Dar es salaam mpaka Dodoma nayo imekamilika na nyote ni mashahidi”amefafanua Mhe. Prof. Mbarawa

Mhe. Prof. Mbarawa amefafanua kuwa  hadi sasa serikali imeendelea kununua vichwa 19 vya umeme na mabehewa 89 ya abiria na vichwa vya mchongoko 10 na hadi sasa serikali imeshapokea vichwa 17 vya umeme mabehewa 65 ya abiria na seti ya treni ya mchongoko 3 .

“Miradi mingine mitatu ya ujenzi wa reli mpya, zenye reli za kisasa yenye uwezo wa kubeba tani 3,500 kwenye ziwa Tanganyika na nyingine ya kubeba tani 3,000 kwenye ziwa Victoria hivi karibuni zitaanza kujengwa, pia kwa mara ya kwanza kwenye historia ya nchi yetu tunajenga kiwanda kikubwa cha kutengenezea Ndege huko Kigoma, chenye uwezo wa kutengeneza Ndege kubwa yenye uwezo wa kubeba tani 5,000 ambayo naamini ujenzi utaanza hivi karibuni” ameeleza Mhe. Prof. Mbarawa.

Mkutano huo unaofanyika kila mwaka tangu kuanzishwa mwaka 2017, umehudhuriwa na wataalamu wa sekta ya uchukuzi na  unajumuisha wanachama wa FEAFFA kutoka nchi za Tanzania, Burundi, Rwanda, Uganda, Kenya na Sudan Kusini, pia nchi ya Afrika kusini na mbalimbali maeneo mbalimbali Duniani.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo