Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MHE. RAIS DK. HUSSEIN ALI MWINYI ATEMBELEA JENGO LA LATRA - SABASABA
Imewekwa: 13 Jul, 2024
MHE. RAIS DK. HUSSEIN ALI MWINYI ATEMBELEA JENGO LA LATRA - SABASABA

Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ametembelea jengo la Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) katika viwanja vya Julius Nyerere - Sabasaba kwenye maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara jijini Dar es Salaam Julai 13, 2024 na kushuhudia shughuli za udhibiti zinazotekelezwa na LATRA.

Akitoa maelezo katika jengo la LATRA, Bw. Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA amesema kuwa, LATRA inatumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utoaji wa huduma kwa wadau wake jambo ambalo limesaidia katika kuongeza ufanisi wa shughuli za kiudhibiti.

Aidha, moja ya Mfumo wa TEHAMA aloutaja Bw. Pazzy ni pamoja na Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) unaosaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto za ajali nchini zinazogharimu maisha ya watanzania na mali zao.

Vilevile Bw. Pazzy ameutaja Mfumo mwingine kuwa ni Mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS) unaomuwezesha abiria kupata taarifa ya basi lilipo, sehemu inayotoka na muda wa kuwasili kituoni na kukagua mwendokasi wa basi alilopanda.

Pia Bw. Pazzy ameeleza kuwa, LATRA na Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani Zanzibar (ZARTSA) zinatarajia kuingia mkataba wa makubaliano katika maeneo ya ushirikiano ya masuala ya kiudhibiti kwa kubadilishana uzoefu katika sekta ya usafiri ardhini.

“Mkataba tutakaoingia utaongeza ufanisi katika sekta ya udhibiti kati ya taasisi hizi na haya ni maazimio ya makubaliano baada ya majadiliano yaliyofanyika wakati wa miaka 60 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar mwezi Januari, 2024” ameeleza Bw. Pazzy.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo