Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MHE. SENYAMULE: LATRA EPUKENI RUSHWA, CHUKUENI HATUA DHIDI YA WAVUNJA SHERIA
Imewekwa: 28 Jan, 2023
MHE. SENYAMULE: LATRA EPUKENI RUSHWA, CHUKUENI HATUA DHIDI YA WAVUNJA SHERIA

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, amewaagiza wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuchapa kazi kwa kuzingatia uweledi, kuepuka vitendo vya rushwa na kuchukua hatua dhidi ya madereva na wasafirishaji wanaokiuka Sheria za matumizi sahihi ya miundombinu ya usafirishaji. Ameyasema hayo tarehe 26 Januari, 2023 katika hafla ya uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi wa LATRA iliyofanyika Makao Makuu ya LATRA jijini Dodoma.

Akizungumza katika hafla hiyo Mhe. Senyamule amesisitiza kuwa Serikali kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi katika maendeleo ya miundombinu ya barabara na reli nchini, hata hivyo kuna baadhi ya madereva na wasafirishaji wanashindwa kutimiza wajibu wao na kusababisha maafa na taharuki kwa watumiaji wengine wa miundombinu hiyo.

Aidha, amesema kuwa mazingira ya wafanyakazi wa LATRA yanavishawishi vingi kutokana na mgongano wa maslahi ya watoa huduma mbalimbali hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa uweledi na uadilifu ili kuboresha huduma inayotolewa kwa wananchi na kuepusha migogoro.

‘Sisi Dodoma tumebahatika kupata miundombinu mizuri ya usafiri wa barabara na reli, LATRA muendelee kutoa elimu ya matumizi sahihi ya miundombinu kwa umakini na kwa kufuata taratibu sahihi ili kukamilisha azma ya Serikali ya kuwezesha maisha bora kwa Watanzania.’ Alisema

Pia ametoa rai kwa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Mawasiliano na Usafirishaji (COTWU) kuleta mshikamano wa wafanyakazi na kushirikiana na menejimenti ili kuongeza tija na kuepusha migogoro mahala pa kazi.

‘Baraza la Wafanyakazi ndio jukwaa la Kisheria la Majadiliano ya pamoja kati ya viongozi wa tasisi na wafanyakazi. Uundwaji wa mabaraza ya wafanyakazi ni agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la mwaka 1970 na ni utekelezaji wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004 kifungu cha 73 kinachoelekeza juu ya kutekeleza sera ya kuwashirikisha wafanyakazi katika maamuzi na ni utawala bora.’ Alisema

Aliongeza kuwa kwa mujibu wa Sheria, Baraza hilo linapaswa kukutana angalau mara mbili kwa mwaka, mara ya kwanza linapopitisha mpango na bajeti ya taasisi na mara ya pili linapofanya mapitio ya utekelezaji wa mpango na bajeti kwa nusu mwaka. Hivyo, amewapongeza washiriki wote kwa kukamilisha taratibu za kisheria kwa kuunda baraza la wafanyakazi lililosajiliwa na Kamishna wa Kazi kwa ujibu wa Sheria.

Wakati huo huo, Mhe. Senyamule ameipongeza LATRA kwa kuhamia Makao Makuu ya Nchi mkoa wa Dodoma na kuwakaribisha katika mkoa huo ulio na fursa lukuki za maendeleo.

‘Nachukua fursa hii kuwakaribisheni sana hapa Dodoma, Makao Makuu ya Nchi yetu. Nafahamu kwamba LATRA ni miongoni mwa Taasisi zilizotekeleza Agizo la Serikali la kuhamia Dodoma, na ninayo taarifa Ofisi yenu ya Makao Makuu ilihamia rasmi Dodoma tarehe 26 Septemba, 2022 ambapo leo tarehe 26 Januari, 2023 mnatimiza miezi minne kamili. Karibu sana Mkurugenzi Mkuu, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa Ofisi ya Makao Makuu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa LATRA CPA Habibu Suluo, amempongeza Mkuu wa Mkoa huyo kwa kusimamia kwa ufanisi maendeleo ya mkoa wa Dodoma na kuwa LATRA itaendelea kushirikiana na Uongozi wa mkoa kuongeza ufanisi katika huduma za usafiri ardhini.

‘Mkoa wa Dodoma unapendeza, ratiba zetu na leseni tunazotoa kwa mabasi zinawezesha usafiri kutoka Dodoma kwenda mikoa yote Tanzania na kufika siku hiyo hiyo.’ Alieleza.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi COTWU, tawi la LATRA Patel Ngereza amesema kuwa, Wafanyakazi wa LATRA wanampongeza Mkurugenzi Mkuu, CPA Habibu Suluo kwa kufanya maboresho makubwa katika utendaji wa Mamlaka ikiwa ni pamoja na kusikiliza na kutatua kero za wafanyakazi, kutekeleza kwa vitendo ushirikishwaji wa wafanyakazi katika uendeshaji wa shughuli za Mamlaka na kushirikisha kwa karibu wadau mbalimbali wakiwemo wasafirishaji, Jeshi la Polisi na taasisi za Serikali tangu alipoteuliwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Julai, 2022.

‘Kutokana na juhudi za uongozi wa LATRA, sisi viongozi tunaendelea kuhamasisha Wafanyakazi wa LATRA kuchapa kazi kwa bidii, ubunifu na kuwajali wateja wetu huku tukiiomba menejimenti kuendelea kutimiza mahitaji ya wafanyakazi katika mahala pa kazi.’ Alisema

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo