Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MHE. SIMBACHAWENE AIPONGEZA LATRA KWA UTENDAJI KAZI NA UBUNIFU WA MFUMO WA PIS
Imewekwa: 20 Jun, 2025
MHE. SIMBACHAWENE AIPONGEZA LATRA KWA UTENDAJI KAZI NA UBUNIFU WA MFUMO WA PIS

Mhe. George Simbachawe (Mb), Waziri wa Nchi, ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, amekoshwa na mfumo wa taarifa kwa abiria (PIS), ambao ni mfumo unaomuwezesha abiria kujua basi lilipo, muda wa kuwasili kituoni na kukagua mwendo kasi wa basi alilopanda

Mhe. Simbachawene ameyasema hayo Juni 16, 2025 alipotembelea banda la LATRA na kupatiwa elimu ya jinsi mfumo huo unavyofanya kazi kwenye maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.

Vilevile Mhe. Simbachawene amesisitiza wadau kutumia mfumo huo wa PIS kwa kuwa itaondoa udanganyifu kwa abiria wanaosafiri kwa njia ya basi, ambapo wataweza kuona  mahali basi lilipo na mwendokasi wa basi husika kwa kutumia simu kiganjani

Akitoa elimu ya mifumo ya kidigitali inayotumiwa na LATRA, Bi. Rukia Kibwana, Afisa Leseni na Usajili LATRA, amesema kuwa, Mfumo wa Taarifa kwa abiria (PIS) umeleta mapinduzi makubwa kwenye sekta ya usafiri ardhini kwa kumuwezesha abiria kuona namna mabasi yanavyoingia na kutoka pamoja na kujua mwendokasi wa basi husika.

 “Mfumo wa Taarifa kwa abiria (PIS) umetokana na mfumo wa kufuatilia mwenendo wa magari (VTS) na tangu kuzinduliwa kwake Julai 2024, mfumo huu umeleta mabadiliko makubwa kidigitali haswa kwenye sekta ya Usafiri Ardhini kwa kuwezesha abiria kuwa na ratiba ya magari yote yanayotoka na kuingia nchini, pamoja na mwendokasi wa basi husika na mpaka sasa umefungwa kwenye stendi kuu mbili ya magufuli mkoani Dar es salaam na nane nane jijini Dodoma”, amesema Bi. Rukia.

Naye Bi. Kibwana aliongeza kuwa mbali na mfumo wa PIS kuna mfumo wa Uthibitishaji wa Madereva (DTS) kuwa ni mfumo wa kielektroniki wa kutahini madereva, ambapo dereva anatakiwa kujisajili kwa kutumia namba yake ya NIDA kwenye mfumo mama wa usimamizi wa taarifa za Barabara na Reli (RRIMS)  na kuweka nafasi ya kufanya mtihani na kisha kuchagua tarehe na muda atakaopenda kufanya mtihani.

LATRA inatekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika jijini Dodoma, inayosema Himiza Matumizi ya Mifumo ya Kidigiti ili kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchagiza Uwajibikaji, ambapo kupitia maadhimisho hayo, LATRA inatoa elimu ya mifumo mbalimbali ya kidigitali inayotumiwa na Mamlaka katika kutekeleza majukumu yake.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo