Bw. Gerson Msigwa, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali amewasihi wamiliki wa vyombo vya usafiri na wasafirishaji kwa jumla kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa na LATRA ili kuwa na sekta ya usafiri ardhini iliyo bora, salama na yenye tija.
Bw. Msigwa amesema hayo hivi karibuni alipotembelea Kituo cha Kufuatilia mwenendo wa magari cha Mamlaka a Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na kujionea jinsi LATRA inavyodhibiti mabasi ya mikoani na nchi jirani yakiwa barabarani kupitia Mfumo wa Kufuatilia Mwendendo wa Mgari (VTS).
Vilevile amesema kuwa, Serikali kupitia LATRA imefanya uwekezaji mkubwa kwa kuwezesha matumizi ya mifumo ya TEHAMA kwa lengo la kuwapa wananchi huduma bora, za uhakika na salama.
“Nataka niwahakikishie kwa uwekezaji uliofanywa kwa LATRA, hakuna kitendo chochote cha uvunjifu wa Sheria na Taratibu za usalama barabarani ambacho kitakuacha salama, ukizidisha mwendokasi, dereva akiendesha hovyo na kufunga breki bila mpangilio tunamuona, chochote kibaya kinachohatarisha usalama wa abiria, kupitia kituo hiki tunakiona na tunachukua hatua,” amesema Msigwa
Aidha, amewaasa wananchi wanaokutana na kadhia pindi wanapotumia usafiri wa umma, kutoa taarifa LATRA kwa namba za bila malipo ambazo ni 0800110019 au 0800110020 ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea.
“Serikali tukipata taarifa kutoka LATRA, kama ni za kwenda polisi, watachukua hatua na kama ni hatua nyingine tutazifanyia kazi kwa mujibu wa Sheria tulizonazo za udhibiti wa usafiri ardhini nchini,” ameeleza Bw. Msigwa
Ameongeza kuwa, Serikali inataka kuona nchi inatoa usafiri ulio bora na salama na kuwaondolea usumbufu watanzania kwa kuwa usafiri ni amani, utalii na burudani. Pia, kwa sasa idadi ya ajali imepungua kutokana na matumizi ya TEHAMA ambapo LATRA, Jeshi la Polisi pamoja na wamiliki wanayafuatilia mabasi yakiwa barabarani na madereva wanajua wanafuatiliwa na hivyo imeongeza nidhamu ya uendeshaji.
Naye CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA amesema LATRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama barabarani wamejipanga kuhakikisha huduma za usafiri zinakuwa salama katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka,
Pia, ameeleza kuwa LATRA inashirikiana na Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), kuhakikisha kila basi linatoa tiketi za kielekroni na kuhakikisha mifumo yote inasomana na LATRA pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
“Kwa sasa watoa huduma 15 mifumo yao inasomana na LATRA na TRA kwa hiyo tunaweza kuona uhalali wa tiketi zinazotolewa kwa abiria,”ameeleza CPA Suluo.