Mhe. David Kihenzile, Naibu Waziri Wizara ya Uchukuzi amekabidhi kadi za utambulisho kwa wahudumu wa mabasi ya abiria 174 waliokidhi vigezo na masharti kati ya wahudumu 798 waliohitimu mafunzo ambapo 728 ni wahitimu kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na wahudumu 70 kutoka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).
Mhe. Kihenzile amekabidhi kadi hizo Novemba 12, 2024 katika hafla ya kwanza ya utoaji kadi za utambulisho kwa wahudumu wa mabasi ya abiria waliohitimu mafunzo na kusajiliwa na LATRA iliyofanyika ofisi za LATRA Dar es Salaam.
“Siku hii ya leo ni muhimu sana katika historia ya Nchi yetu na hususan Sekta ya Uchukuzi kwani kwa mara ya kwanza tunashuhudia LATRA ikitekeleza kifungu cha 5(1)(e) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura ya 413 iliyopitishwa na Bunge la Tanzania Mwaka 2019 na Kanuni za Uthibitishaji wa Madereva na Usajili wa Wahudumu za Mwaka 2020 kwa kuwezesha mafunzo ya Wahudumu wa Mabasi nchini. Natoa kongole kwa wote waliofanikisha suala hili,” amesema Mhe. Kihenzile.
Vilevile Mhe. Kihenzile amewataka wahudumu kujitokeza kwa wingi kupatiwa mafunzo na wale waliofanikisha mafunzo hayo amewataka kuwa mfano bora kwa wengine,”Niwahakikishie kuwa kadi hizi za utambuzi zitasaidia kurasimisha ajira zenu ili ziheshimike kama zilivyo kazi zingine, kuboresha vipato vyenu kwani thamani yenu kwenye soko la ajira ya usafirishaji itaongezeka. Vilevile kadi hizi zitawezesha taasisi zinazoshughulikia masuala ya ajira kuwa na taarifa sahihi zinazowezesha kusimamia maslahi ya wahudumu.” Ameeleza Mhe. Kihenzile.
Aidha amewataka watoa huduma wa vyombo vya moto kibiashara kuacha kuajiri watoa huduma ambao hawajapitia mafunzo kwakuwa inarudisha nyuma jitihada za Serikali na za sekta binafsi katika kuboresha huduma za usafiri nchini.
Naye Prof. Ahmed Mohamed Ame, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi LATRA, amesema kuwa, LATRA imepewa jukumu la kuhakikisha kwamba watanzania wanapatiwa huduma bora za usafiri ardhini zinazotolewa na wahudumu wenye weledi waliopata mafunzo sahihi yenye kuzingatia Sheria,Kanuni na Taratibu zilizowekwa na kisha kusajiliwa na LATRA
Aidha Prof. Ame amezitaja faida za kuwa na wahudumu waliosajiliwa na LATRA ambazo ni; Wamiliki kupata wasimamizi mahiri na wenye weledi wa kazi waliyopewa, Wahudumu kufanya kazi kwa weledi, umakini na ufanisi zaidi, Kuboresha huduma za usafiri ardhini, Kurasimisha kazi ya uhudumu, Kulinda mitaji ya wamiliki wa vyombo na vipato vya wahudumu, Kuwezesha taasisi zinazoshughulikia masuala ya ajira kuwa na taarifa sahihi zinazowezesha kusimamia maslahi ya wahudumu katika ajira na Kuongeza nidhamu na uwajibikaji kwa wahudumu na watumiaji wa huduma.
Pia amewasihi watoa huduma za usafiri wa abiria kuwapatia muda sahihi wahudumu kuhudhuria mafunzo kabla Mamlaka haijaanza kuchukua hatua kwa watoa huduma hao kutumia wahudumu ambao hawajasajiliwa.
“Muda wowote kuanzia sasa tutaanza kuchukua hatua dhidi ya wamiliki watakaotumia wahudumu ambao hawajasajiliwa na kwa upande mwingine wahudumu ambao hawajasajiliwa hawataruhusiwa kutoa huduma kwenye mabasi. Hivyo, kila mdau ahakikishe anatakeleza matakwa ya Sheria na Kanuni zilizopo katika utoaji wa huduma za usafirishaji abiria nchini,” amesema Prof. Ame.
Bi. Gift Benard, Mhudumu wa mabasi ya abiria ameishukuru LATRA kwa kuwawezesha kuwa wahudumu bora na amewaomba waajiri wao (wamiliki wa mabasi) kuwawezesha kupata mkataba katika ajira yao.
Mtaala wa kutoa mafuzo ulizinduliwa rasmi tarehe 1 Julai, na mafunzo hayo yalianza rasmi Novemba 22, 2023 katika chuo cha CBE na NIT.