Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

PAZZY: WAPIGIENI KURA WASAFIRISHAJI BORA WA MABASI
Imewekwa: 15 Aug, 2024
PAZZY: WAPIGIENI KURA WASAFIRISHAJI BORA WA MABASI

Bw. Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amewasihi wadau wa usafiri ardhini kupiga kura kwa kujaza dodoso kupitia kiunganishi https://forms.edodoso.gov.go.tz/x/Othf4u0Q ili kuchagua wasafirishaji bora na salama wa mabasi ya masafa marefu nchini na yanayoenda nchi jirani, na  mwisho wa kupiga kura ni tarehe 19 Agosti, 2024.

Akizungumza na wanahabari Agosti 14, 2024 katika ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Pazzy amesema kuwa, Mamlaka imeandaa tuzo za LATRA kwa Wasafirishaji Bora na Salama kwa Mabasi ya Mikoani na Nchi Jirani ili kuhamasisha na kuchochea matumizi ya mifumo ya utoaji wa huduma bora na salama ya usafirishaji wa abiria kwa ufanisi na ubunifu hususan katika matumizi ya teknolojia.  

Vilevile amesema, Mamlaka imeandaa tuzo za Wasafirishaji Bora na Salama kwa huduma za mabasi zilizotolewa kuanzia tarehe 01 Julai 2023 hadi 30 Juni 2024 na Washindi watakabidhiwa tuzo katika Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani yatakayofanyika tarehe 26 hadi 30 Agosti 2024 Mkoani Dodoma.

Aidha, Bw. Pazzy ameeleza kuwa Mamlaka itazingatia vigezo mbalimbali vitakavyotumika kupata washindi ikiwemo usalama wa huduma inayotolewa, uhakika wa huduma inayotolewa, ubunifu na matumizi ya teknolojia katika utoaji huduma ambayo itawafurahisha abiria na msafirishaji anayetoa huduma iliyokuwa endelevu na uhakika kwa abiria.

“Watumia huduma na wadau wote mnaombwa kushiriki kwa kuwapigia kura wasafirishaji kwa kuzingatia huduma zilizotolewa kwa kipindi husika. Vigezo na jinsi ya kupiga kura vinapatikana kupitia tovuti ya Mamlaka www.latra.go.tz  kurasa za mitandao ya kijamii za LATRA au kiunganishi https://forms.edodoso.gov.go.tz/x/Othf4u0Q,” amesisitiza Bw. Pazzy.

Vilevile amefafanua kuwa, washindani wamegawanywa katika makundi matatu ambayo ni Wasafirishaji Wakubwa (wenye mabasi zaidi ya 30), Wasafirishaji wa Kati (wenye mabasi 11 hadi 30) na Wasafirishaji Wadogo (wenye mabasi matatu hadi 10).

Kifungu cha 6(a) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura ya 413, pamoja na mambo mengine, kinaeleza kuwa Mamlaka ina wajibu wa kuhamasisha ushindani wenye ufanisi miongoni mwa watoa huduma zinazodhibitiwa, na uandaaji wa tuzo hizo ni sehemu ya utekelezaji wa jukumu hilo.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo