
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetengeneza Mfumo wa Taarifa kwa Abiria (Passenger Information System -PIS) unaomuwezesha mwananchi kutambua muda ambao basi la masafa marefu litafika katika stendi ya mabasi aliyoichagua pamoja na kufahamu mwendo wa basi husika pindi akiwa safarini.
Akizungumza baada ya kutembelea Jengo la LATRA kwenye Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (sabasaba), viwanja vya Julius Nyerere na kupatiwa elimu kuhusu mfumo huo, Mhe. Sophia Mwakagenda, Mbunge wa viti maalum Mbeya, ameipongeza LATRA kwa kutumia vizuri Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utekelezaji wa majukumu yao kwa wananchi.
“Nitoe pongezi nyingi kwa LATRA kwa kuja na mfumo huu, nimejifunza vitu vingi hususan maendeleo ya kidigitali kwani naweza kutambua ndugu yangu yuko sehemu gani kwa kuangalia kupitia simu janja yangu na hakuna haja ya kufika stendi na kumsubiri mgeni wako kwa muda mrefu,” ameeleza Mhe. Mwakagenda.
Mhe. Mwakagenda ameongeza kuwa, Mfumo wa PIS unasaidia sana kupunguza mabasi kutembea mwendo hatarishi na unaisaidia LATRA kubaini na kusimamia muda wa basi kufika katika kila kituo kwa mujibu wa ratiba walizopatiwa.
Naye CP Awadhi Haji, Mkuu wa Oparesheni na Mafunzo kutoka Jeshi la Polisi Tanzania, ameipongeza Mamlaka kwa ubunifu unaoendana na ukuaji wa teknolojia unaoweza kutatua changamoto mbalimbali za wananchi.
Akizungumza na wadau wa usafiri ardhini waliotembelea jengo la LATRA kwenye Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) Dar es Salaam, CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA mesema Mfumo huo unamuwezeshe mwananchi kuwa na taarifa kwa ukaribu zaidi kuhusiana na mwenendo wa mabasi yanayowasili katika vituo mbalimbali nchini.
“Kwa sasa kama una ndugu yako anatoka safari, huna haja ya kumpigia simu kufahamu alipo, bali utaingia kwenye mfumo, cha msingi ufahamu namba ya basi alilopanda. Vivyo hivyo kwa abiria akitumia mfumo huu wa PIS hatokuwa na haja ya kuuliza mahali alipo au muda anaotarajia kufika aendako,” amesema CPA Suluo.
Vilevile ameongeza kuwa, kwa sasa mfumo wa PIS upo katika runinga zilizofungwa kwenye stendi ya mabasi Magufuli Dar es Salaam na stendi ya mabasi nanenane jijini Dodoma, lakini pia mfumo huo unapatikana kwa anwani ya https://pis.latra.go.tz/ kupitia simu janja au komputa, na amewasihi wananchi kutumia mfumo huo utakaowapa taarifa sahihi pindi wawapo safarini au wanapomsubiri msafiri katika stendi mbalimbali za mabasi ya masafa marefu.
Bi. Anna Joseph ni mmoja wa wadau waliotembelea jingo la LATRA katika Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (sabasaba) na amesema kuwa, amefurahishwa sana na mfumo wa PIS ambao unarahisisha muda na kuwapa uhakika wa safari abiria pindi wanapotaka kusafiri, “kwa sasa hata kama sipafahamu ninapokwenda, kupitia mfumo huu wa PIS nitakuwa naangalia vituo mpaka pale nitakapofika safari yangu, pia nimefurahi naweza kuona mwendo wa basi niwapo safarini na nikiona mwendo ni mkubwa nitakuwa namwambia dereva na kondakta wake ili apunguze.”
Kwa upande wake, Mha. Eliud Kataraihya, Mkuu wa kitengo cha TEHAMA kutoka LATRA amesema, Mamlaka itaendelea kubuni mifumo mbalimbali itakayomsaidia mwananchi na itakayorahisisha kazi ya udhibiti kwa Mamlaka.
Mfumo huo mpya wa PIS umezinduliwa rasmi kwenye Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (sabasaba) katika viwanja vya Julius Nyerere yanayofanyika kwa siku 16 kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, 2024 na katika maonesho hayo, wadau mbalimbali wa usafiri ardhini wameonesha kuvutiwa na kufurahia mfumo huo.