Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

PROF. AME AHIMIZA MAADILI, KUCHAPA KAZI NA MATUMIZI YA TEHAMA
Imewekwa: 08 Feb, 2023
PROF. AME AHIMIZA MAADILI, KUCHAPA KAZI NA MATUMIZI YA TEHAMA

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya LATRA Prof. Ahmed Mohammed Ame aliyeteuliwa tarehe 15 Januari, 2023 ameongoza kikao cha Bodi ya Wakurugenzi kilichofanyika Februari 7, 2023 LATRA Makao Makuu jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa kikao hicho Prof. Ame alisema kuwa anamshukuru Mwenyezi Mungu na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumuamini katika nafasi hiyo. 

Aidha, amewakumbusha wajumbe wa menejimenti na wafanyakazi wa LATRA kuchapa kazi kwa kuzingatia maadili na ubunifu ikiwemo matumizi ya mifumo ya TEHAMA ili kuongeza tija katika kuwahudumia Watanzania.

Pia amewasihi wajumbe wa Menejimenti kuimarisha ushirikishwaji wa wafanyakazi katika ngazi mbalimbali za maamuzi ikiwemo baraza la wafanyakazi na viongozi kujishusha ili wafanyakazi watoe mawazo yao kwa uhuru.

"Ratiba ya vikao vya baraza la wafanyakazi ijulikane mapema na iheshimiwe, haipendezi kubadilisha tarehe ya mkutano wa baraza kwa kuwa wafanyakazi huwa wanajipanga kuwasilisha hoja mbalimbali na ukibadilisha ratiba huwa wanajisikia kutothaminiwa". Alifafanua 

Aidha, amesisitiza Mamlaka kuzingata usawa wa kijinsia katika kuajiri wafanyakazi kwa kutoa kipaumbele kwa wanawake wenye sifa zinazohitajika ili kuboresha uwiano wa kijinsia.

Kuhusu ushiriki wa wafanyakazi katika michezo, Mwenyekiti huyo wa Bodi amesisitiza wafanyakazi washiriki katika michezo na kuongeza kuwa yeye ni mpenzi wa michezo na akipata wasaa atashiriki katika michezo itakayoandaliwa.

Vilevile amesisitiza kufanya kazi kwa ukaribu na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa watoa huduma zinazodhibitiwa.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo wa Bodi ametoa shukrani kwa wajumbe wa Bodi anayoiongoza, Menejimenti na Wafanyakazi wa LATRA na wadau wengine kwa salamu za pongezi na mapokezi mazuri aliyoyapata.

Kwa upande wake, Prof. Ame ameahidi kushirikiana na wajumbe wa Bodi hiyo na Menejimenti ili kuhakikisha kuwa malengo ya Mamlaka hiyo yanatekelezwa.

"Tutafanya kazi kuwa kushirikiana, panapohitaji kukumbushana tutakumbushana na panapohitaji kukosoana tutakosoana". Alisema

Akizungumza kwa niaba ya Mhandisi Dkt John S. Ndunguru, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bodi hii , Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya LATRA Wakili Tumaini Silaa alimkaribisha Prof. Ame na kumuahidi ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake.

Aidha, alimkabidhi , Sheria ya LATRA Sura ya 413 na Kanuni zake, Sheria ya Leseni za Usafirishaji na Kanuni zake na Sheria ya Reli ikiwa ni sehemu ya vitendea kazi vitakavyotumika kutekeleza majukumu ya bodi hiyo

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo