Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

SACCOS YA KWANZA YA MAAFISA UFARISHAJI KUANZISHWA MKOANI NJOMBE
Imewekwa: 18 Jan, 2026
SACCOS YA KWANZA YA MAAFISA UFARISHAJI KUANZISHWA MKOANI NJOMBE

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Njombe imeanza utekelezaji wa mpango wa kuanzisha Chama cha Ushirika (SACCOS) cha kwanza cha maafisa usafirishaji wa Pikipiki za magurudumu mawili (Bodaboda) na magurudumu matatu (Bajaji) Mkoani Njombe hatua inayolenga kurasimisha shughuli za bodaboda na b ajaji na kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi kupitia SACCOS.

Hayo yamebainishwa na Mhe. Anthony Mtaka, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Januari 6, 2026 wakati CPA, Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi mkuu LATRA alipofanya ziara mkoani Njombe kwa lengo la kukutana na kuzungumza na maafisa usafirishaji wa pikipiki za magurudumu mawili na matatu. Mhe. Mataka amesema kuwa, wazo la LATRA la kuanzisha SACCOS ni kubwa na linakwenda kutoa suluhisho la muda mrefu katika sekta ya usafirishaji Mkoa wa Njombe.

“Wazo hili litawezesha kazi ya Bodaboda na Bajaji kurasimishwa kama kazi nyingine kupitia SACCOS inayoenda kuanzishwa, wasafirishaji wataweza kujiwekea akiba zao, kuongeza kipato na kupata huduma za bima kama zilivyo ajira nyingine. Na Serikali ya Njombe ipo tayari kushirikiana na LATRA kuhakikisha SACCOS itakayoenda kuanzishwa inakuwa ya mfano wa kuigwa kitaifa na kuwa chombo muhimu cha kuwawezesha wasafirishaji kujikwamua kiuchumi,” amesema Mhe. Mtaka”.

Kwa upande wake CPA, Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA, amesema Mamlaka imeweka mkakati maalum wa kuwaangalia kwa karibu vijana wa sekta ya usafirishaji Mkoa wa Njombe kwa lengo la kuboresha huduma za usafiri mkoani hapo.

“SACCOS hii inayoanzishwa Njombe itakuwa ya kwanza na ya mfano katika mkoa huu, mtazamo wetu ni kuwa na mfumo wa kidijiti utakaowaunganisha vijana wote wa usafirishaji kuanzia ngazi ya Mkoa, Wilaya hadi Kata, utakaowawezesha kujitambua, kupata taarifa zao kwa urahisi na hatimaye kuunganishwa katika Mfumo wa Kitaifa, hatua itakayoboresha huduma za usafiri na kuongeza uwajibikaji kupata ushirikiano wa pamoja,” amesema CPA, Dkt. Suluo.

Ameongeza kuwa, Sheria ya LATRA imebaini umuhimu wa wasafirishaji wa Pikipiki za magurudumu mawili na matatu kujiendesha na kujisimamia wenyewe, hivyo kupendekeza uwepo wa vyama vya ushirika ambavyo baada ya kupitishwa kwa Kanuni husika, LATRA imeendelea kutoa elimu na kuhamasisha uundaji wa SACCOS.

“Kabla ya kuwapatia uwakala wasafirishaji wanawasilisha maombi LATRA kupitia Mfumo wa Usimamizi na Utoaji Leseni za Usafiri wa Barabara na Reli (RRIMS) unaopatikana kwa anwani ya https://rrims.latra.go.tz/ na tukiridhika kuwa vigezo vimetimizwa, wanaanza kufanya kazi kupitia mfumo. Mapato yao yanaingia kwenye Mfumo wa LATRA kupitia namba ya malipo (control number) na kila mwezi tunawarejeshea asilimia 20 ya mapato wanayokusanya,” amesema CPA, Dkt. Suluo.

Naye Dkt. Fredy Msemwa, Katibu Mtendaji Tume ya Taifa ya Mipango, amesema mpango wa kuanzishwa kwa SACCOS unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, yenye lengo la kuchochea urasimishaji na kukuza sekta ndogo ya ushirika nchini.

“Kupitia SACCOS zitakazoanzishwa, vijana wa bodaboda wataweza kutambuliwa rasmi, kuweka malengo ya maendeleo na kupata fursa za kiuchumi ambazo mtu mmoja mmoja asingezifikia,” amesema Dkt. Msemwa.

Vilevile amesema kuwa, Tume ya Taifa ya Mipango iko tayari kufanya kazi kwa karibu na LATRA kuhakikisha mpango wa uanzishwaji wa SACCOS unafanikiwa, hususan katika kuwaunganisha vijana katika mifumo ya akiba na kuwawezesha ujisimamia kiuchumi.

Kwa upande wake Bw. Vermud Msigwa, Mwenyekiti wa Maafisa Usafirishaji Mkoa wa Njombe, ameishukuru Serikali na LATRA kwa fursa ya mchakato wa kuanzisha SACCOS mkoa wa Njombe kuwa utawasaidia wasafirishaji kusaidiana wenyewe kwa wenyewe na kupata mikopo yenye riba nafuu isiyo na masharti kandamizi.

LATRA inaendelea kusisitiza ushirikiano wa wadau wote kuhakikisha sekta ya usafiri wa pikipiki za magurudumu mawili na matatu inakuwa rasmi, salama, yenye tija na inayochangia maendeleo ya vijana na taifa kwa jumla.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo