Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

SAFARI SAA 24 RUKSA KUANZIA OKTOBA 1, 2023
Imewekwa: 29 Sep, 2023
SAFARI SAA 24 RUKSA KUANZIA OKTOBA 1, 2023

Serikali imetangaza rasmi kuanza kutolewa kwa ratiba za mabasi ya abiria kusafiri kwa saa 24 kuanzia tarehe 1 Oktoba, 2023

Kauli hiyo imetolewa na Mhe. Jumanne Sagini (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Golden Tulip jijini Dar es Salaam, Septemba 29, 2023.

Mhe. Sagini amesema kuwa, Serikali inataka kuona usafiri wa saa 24 unakuwa salama na wenye ufanisi huku akiitaka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kutoa ratiba za saa 24 kwa kuwashirikisha watoa huduma na kuhakikisha Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) unafanya kazi muda wote.

Akieleza sababu za kuanza kwa huduma hizo za saa 24, Mhe Sagini ameeleza kuwa, tathimini iliyofanyika imeonesha kuwa udhibiti wa hali ya usalama umeimarika kupitia Jeshi la Polisi, wananchi wamebadilika kitabia na kuanza kuhifadhi pesa zao benki hivyo hawatembei na pesa taslimu, huduma za mawasiliano ya simu zimeboreshwa, LATRA imesimika mfumo madhubuti wa kufuatilia mwenendo wa magari (VTS), miundombinu ya barabara imeimarika na wasafirishaji wapo tayari kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa,

Aidha, Mhe. Sagini ametoa maelekezo mahususi kwa wasafiri na wasafirishaji, “ Wamiliki wa mabasi wanatakiwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu kwa mujibu wa leseni zao na Madereva wa mabasi wanapaswa kuthibitishwa na LATRA kwa mujibu wa kanuni zilizopo”

Vilevile amesema kuwa, “TAMISEMI ihakikishe kunakuwepo na huduma za msingi hasa katika stendi za mabasi na  Jeshi la polisi liendelee kulinda watu na mali zao wakati wote, usiku na mchana na kuimarisha doria katika maeneo ya stendi, barabara kuu na barabara za mikoa na kuhakikisha Sheria za Usalama Barabarani zinazingatiwa na kila mdau.”

Naye Bw. Johansen Kahatano, Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara kutoka LATRA amesema Mamlaka imejipanga kikamilifu kusimamia safari za saa 24 kwa kuweka mikakati thabiti itakayowezesha safari hizo kuwa na tija katika maendeleo ya Taifa huku usalama ukiwa ni kipaumbele.

“Kwa upande wetu tunayo nguvu ya kutosha ili kusimamia eneo hili, hivyo niwakaribishe wasafirishaji ambao wana nia ya kufanya safari hizi watume maombi, mpaka sasa tuna maombi ya makampuni 7 yanayotaka kufanya safari hizi. Katika kusimamia huduma hizi, wasafirishaji watasaini tamko ambalo litaelezea ulazima wa madereva kuwa wamesajiliwa, kuwa na mtu maalumu ambaye atasimamia magari haya usiku, taarifa sahihi za abiria kuwepo kwenye mfumo wa Tiketi Mtandao pamoja na kuweka utambulisho maalum wa mizigo ya abiria,” amesema Bw. Kahatano.

Kwa upande wake, SACP Ramadhani Ng’anzi, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani amesema kuwa Jeshi hilo litaendela kuhakikisha usalama wa raia na mali zao mahali popote ili kufanya nchi iwe salama.

Safari za saa 24 zilisitishwa kwa agizo la Serikali mwaka 1994 kutokana na sababu mbalimbali kama vile; hali ya usalama wa raia na mali zao, miundombinu mibovu na ajali zilizokuwa zinasababisha madhara makubwa kwa binadamu. Hata hivyo, Serikali kupita LATRA ilianza kuruhusu safari kuanzi saa 11 alfajiri na baadae saa 9 alfajiri ili kujiridhisha na udhibiti wa safari hizi na hatimaye safari za saa 24 zimeruhusiwa. Umetolewa wito kwa watumiaji wa huduma za usafiri nchini (wasafirishaji na abiria) kuzingatia Sheria za Usalama Barabarani ili kuhakikisha faida zilizotazamiwa kwenye safari hizi zinafikiwa kikamilifu.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo