Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

SEKTA BINAFSI SHIRIKINI UJENZI WA MIUNDOMBINU - PROF. MBARAWA
Imewekwa: 16 Nov, 2022
SEKTA BINAFSI SHIRIKINI UJENZI WA MIUNDOMBINU - PROF. MBARAWA

Na Mambwana Jumbe

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amezungumzia umuhimu wa sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika ujenzi wa miundombinu ili kuharakisha maendeleo na kukuza uchumi wa taifa na mtu mmoja mmoja.

Akifungua mkutano wa 15 wa mwaka wa wadau wa sekta ya uchukuzi wenye lengo la kufanya tathmini kuhusu maendeleo ya sekta hiyo nchini, Prof. Mbarawa amesema ushiriki wa sekta binafsi, Serikali na wadau wa maendeleo utaharakisha ujenzi wa reli, barabara, viwanja vya ndege na meli na hivyo kutoa fursa nyingi za ajira na kuhuisha miundombinu ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa taifa.

“Serikali tumejipanga kushirikiana na sekta binafsi katika ujenzi wa barabara mpya ya Kibaha-Chalinze-Morogoro kilomita 215 (express way), ambapo mkandarasi atajenga kwa fedha yake na watakaotumia barabara hiyo watalipia,” amesema Prof. Mbarawa. 

Amebainisha kuwa Serikali inajipanga kubadilisha Sheria ya TAZARA na TRC ili kuwezesha sekta binafsi kushiriki katika huduma ya usafiri wa reli kwa kununua mabehewa na kuyaendesha. 

Amezungumzia umuhimu wa Tanzania kuwa na miundombinu bora kwa haraka ili kumudu kuhudumia kikamilifu soko la ndani na nchi sita ambazo hutegemea huduma ya uchukuzi kutoka Tanzania, ambazo ni Malawi, Zambia, Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Kingdom Mbangula akizungumzia ujenzi wa barabara mpya ya kulipia, amesema barabara hiyo itakuwa na njia nne, mbili kwenda Morogoro na Mbili kurudi Kibaha na magari hayatapishana ili kuepusha msongamano na ajali.

“ TANROADS tumejipanga ipasavyo kuhakikisha mradi huu unajengwa kwa ubora uliokusudiwa na kukamilika kwa wakati,” amefafanua Eng. Mbangula.

Naye Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Patricia Laverley ameishukuru Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi  kwa kuandaa mkutano huo wa tathmini wa kila mwaka ambao unaibua changamoto na kuzipatia ufumbuzi kwa haraka.

Amesisitiza kuwa AfDB imetenga asilimia 60 ya bajeti yake katika uwezeshaji ujenzi wa miundombinu ili kuchochea maendeleo ya uchumi kwa nchi za Afrika. 

Katibu Mkuu sekta ya Uchukuzi Bw. Gabriel Migire amesema mkutano huo pamoja na mambo mengine utaibua hoja mbalimbali zinazolenga kuboresha sekta ya uchukuzi nchini hivyo kuvutia wawekezaji wengi kupitisha mizigo yao Tanzania na hivyo kukuza uchumi wa taifa.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo