Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

SILANDA: TUMIENI SACCOS KUJIKWAMUA KIJAMII NA KIUCHUMI
Imewekwa: 16 May, 2023
SILANDA: TUMIENI SACCOS KUJIKWAMUA KIJAMII NA KIUCHUMI

Meneja Uratibu Usalama na Mazingira kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Bw. Geoffrey Silanda amewaasa wamiliki na madereva wa pikipiki za magurudumu Mawili (Bodaboda) na Matatu (Bajaji) kutumia vizuri Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) ili kujikwamua kijamii na kiuchumi.

Bw. Silanda amesema hayo wakati akifunga mafunzo ya Ushirika kwa wanachama wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) kwa wamiliki na madereva wa pikipiki za magurudumu mawili (boda boda) na pikipiki za magurudumu matatu (bajaji) katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mjini na Moshi Vijijini uliofanyika Mei 16, 2023 katika ukumbi wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Manispaa ya Moshi mjini Mkoani Kilimanjaro.

“kwa kupitia ushirika huu, mtapata manufaa mengi ikiwa ni pamoja na fursa ya kujiwekea taratibu za utoaji huduma za usafirishaji, kupata mitaji kwa ajili kuboresha au kuongeza huduma, kunzisha miradi mbalimbali ya maendeleo, kujikwamua kutoka kwenye kuajiriwa mpaka kujiajiri kwa kuweza kununua bajaji na bodaboda zenu wenyewe pamoja na kupata elimu ya mara kwa mara ya biashara, usalama barabarani na masuala mengine ikiwemo kukopeshana vitendea kazi,” amesema Bw. Silanda.

Vilevile amesema kuwa, Mamlaka inafanya jitihada kubwa  kuboresha sekta ya usafiri wa bodaboda na bajaji na moja ya jitihada ni kusaidia uanzishwaji wa vyama vya ushirika kwa wamiliki na madereva wa vyombo hivyo, “Niwahakikishie kuwa Mamlaka ipo pamoja na ninyi wanaushirika katika kuhakikisha chama kinaleta manufaa chanya kwenu ninyi. Katika hili tumekuwa pamoja kuanzia upokeaji wa taarifa ya kamati ya uratibu kuhusu uanzishwaji wa ushirika huu, tukazindua mafunzo kwa pamoja na leo tunahitimisha mafunzo yetu kwa pamoja.”

Naye Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoani Kilimanjaro SSP. Pili Misungwi amewakumbusha madereva bodaboda na bajaji kuzingatia Sheria za Usalama barabarani ili kuwa na usafiri salama na wenye tija nchini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa wamiliki wa bodaboda na bajaji Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Hamad Bendera ameishukuru LATRA kwa kuratibu uanzishwaji na mafunzo  ya SACCOS hiyo na wameahidi kuwa mfano bora kwa kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Bw. Mohammed Nkya ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Uratibu wa Mchakato wa Uanzishwaji SACCOS hiyo amesema wataendelea kushirikiana na wamiliki na madereva wa bajaji na bodaboda Mkoani hapo na kuhakikisha wanafanikisha azma ya uanzishwaji wa SACCOS hiyo..

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo